Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Maadhimisho ya siku ya wachangia damu
duniani yanalenga kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuchangia damu
kwa hiari pamoja na kuwatambua na kuwaenzi wachangia damu wa hiari.
Meneja wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama Nyanda za Juu Kusini |
Kauli hiyo imetolwa na Meneja wa Mpango
wa Taifa wa Damu Salama kanda ya nyanda za juu kusini, Dkt. Kokuhaba Mukurasi
alipokuwa akifafanua umuhimu wa maadhimisho ya siku ya wachangia damu duniani
maadhimisho yaliyofanyika ngazi ya kanda katika mkoa wa Iringa.
Amesema kuwa maadhimisho hayo
yanalenga kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuchangia damu kwa
hiari na kuwatambua, kuwaenzi na kuwashukuru wachangia damu kwa hiari mara kwa
mara bila ya malipo yoyote.
Dkt. Mukurasi amesema kuwa
maadhimisho ya siku ya wachangia damu duniani mwaka 2014 yanaongozwa na
kaulimbiu isemayo “damu salama uhai wa mama”. Amesema kaulimbiu hiyo ni muhimu
kutokana na ukweli kuwa zaidi ya asilimia 30 ya damu salama hutumiwa na akina
mama wajawazito wanapopata matatizo ya uzazi ikiwa ni pamoja na kutoka damu
nyingi kabla na baada ya kujifungua, mama anapofanyiwa upasuaji na mimba inapotoka.
Meneja wa kanda amesema kuwa mama na
mtoto hutumia zaidi ya asilimia 80 ya tiba ya damu salama hivyo mahitaji hayo
yanaonesha umuhimu wa kuwepo kwa uhakika wa damu salama katika hifadhi ya damu.
Akiongelea mahitaji ya damu salama
kwa kanda ya nyanda za juu kusini, Meneja wa Taifa wa Mpango wa Damu Salama
amesema kuwa kanda hiyo inahitaji wastani wa chupa za damu 28,000 kwa mwaka. Amesema
kuwa kanda hiyo hukusanya wastani wa chupa 19,331 kwa mwaka ikiwa ni wastani wa
asilimia 70 tu na kuelezea kuwa uhitaji bado ni mkubwa.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Gerald Guninita |
Akitoa shukrani kwa makundi
mbalimbali ya kijamii, Gerald Guninita aliyemuwakisha mkuu wa mkoa wa Iringa
ameyapongeza makundi yote ya kijamii, kidini, wanafunzi na wananchi wa mkoa wa
Iringa waliojitolea damu kwa hiari mara kwa mara. Amesema kuwa damu inayokusanywa
na Mpango wa Taifa wa Damu Salama hutolewa bila malipo katika vituo vinavyotoa
tiba ya damu.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni