Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Serikali itaendelea kutengeneza
mazingira mazuri ya ushirikiano na wadau wa maendeleo kwa lengo la
kuwahakikishia huduma bora za matibabu wananchi wa Iringa.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (kulia) na mwakilishi wa hospitali ya Vicenza Dkt. Oscar Banzato |
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa
wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alipokuwa akipokea vifaa tiba vilivyotolewa
kwa msaada na hospitali ya Vicenza ya nchini Italia katika hospitali ya rufaa
ya Iringa.
Dkt. Ishengoma amesema kuwa serikali
itaendelea kutengeneza na kuimarisha mazingira mazuri ya kuwezesha ushirikiano
na wadau wa maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa mkoa wa Iringa na taifa kwa
ujumla. Amesema kuwa ni matumaini yake kuwa ushirikiano huo utaendelea
kuimarishwa na kudumishwa ili uweze kunufaisha wananchi wengi.
Mwakilishi wa hospitali ya Vicenza
toka nchini Italia Dkt. Oscar Banzato ameihakikishia serikali kuwa ushirikiano
baina ya Italia na hospitali ya Vicenza utaendela kuimarishwa ili kuiwezesha
hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa kutoa tiba kwa urahisi kwa wananchi wa
mkoa wa Iringa na wengine watakaopita katika hospitali hiyo.
Dkt. Oscar Banzato |
Katika taarifa ya hospitali ya rufaa
ya mkoa wa Iringa iliyowsilishwa mganga mfawidhi Dkt. Deogratius Manyama
amesema kuwa mkataba wa kwanza wa ushirikiano baina ya hospitali ya rufaa ya
mkoa wa Iringa na hospitali ya Vicenza ya mkoa wa Veneto nchini Italia
ulisainiwa mwezi Oktoba, 2006. Amesema kuwa mkataba huo uliokuwa na thamani ya
Euro 985,000 ulilenga uboreshaji wa ubora wa utoaji wa huduma za afya
zinazotolewa kwa wakazi wa mkoa wa Iringa. Amevitaja vipengele vya mkataba huo
kuwa ni kuboresha miundombinu ya hospitali ya rufaa ya mkoa. Vipengele vingine
amevitaja kuwa ni kuisaidia hospitali ya rufaa ya mkoa kupata vifaa vya kisasa
na kutoa msaada wa kitaalamu kwa hospitali ili kuboresha ubora wa huduma.
Akiongelea utekelezaji huo, Dkt.
Manyama amesema kuwa hospitali ya Vicenza tayari imekamilisha ujenzi wa jengo
la kujifungulia wajawazito ambalo limeanza kutumika tangu mwezi Agosti, 2011. Ameongeza
kuwa ujenzi wa wodi ya watoto pia umekamilika na kuanza kutumika tangu mwezi
Septemba, 2013.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni