Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wananchi mkoani Iringa wametakiwa
kutunza mazingira na kusimamia sheria zilizopo kwa lengo la kuhakikisha vyanzo
vya maji vinalindwa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa
wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alipokuwa akizindua jumuiya ya watumia maji
wa bonde dogo la mto Mfyamba katika kijiji cha Sadani wilayani Mufindi.
Dkt. Ishengoma amesema “kila mmoja
wetu ni shahidi wa uharibifu wa mazingira katika mto wetu, ninapenda
kuwakumbusha kuwa ni jukumu letu sote kutunza na kuhifadhi mazingira na
kubadilisha hali hiyo kwa kuacha kuchepusha maji kinyume na sheria, kuchimba
mchanga na mawe jirani na mto na katika vyanzo vyingine vya maji vinavyoingia
katika mto Mfyamba na kusababisha uchafuzi wa maji hivyo kuhatarisha afya za
binadamu na viumbe walioko majini”.
Aidha, amewataka wananchi kuacha kilimo cha
kiangazi kiitwacho vinyungu kando kando ya mto na vyanzo vingine vinavyoingiza
maji katika mto Mfyamba, ukataji ovyo wa miti rafiki na maji na shughuli za
uchimbaji wa madini mahususi katika kijiji cha Ihanzutwa.
Akiongelea umuhimu wa mto Mfyamba,
Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa shughuli nyingi za kujipatia kipato na
chakula katika eneo linalozunguka mto huo hutegemea sana uwepo wa mto huo.
Amesema kuwa mto huo utakapoharibiwa utahatarisha upatikanaji wa maji na afya
za wananchi wanaotumia maji yam to huo.
Akionesha msisitizo, Dkt. Ishengoma
amepiga marufuku shughuli zote za kibinadamu kama ufyatuaji tofali, kilimo cha
bustani, ufugaji holela, uoshaji wa magari na utupaji taka katika au kando
kando ya vyanzo vya maji.
Afisa wa bonde la Rufiji, Idris Msuya
amesema kuwa kuundwa kwa vyama vya watumia maji ni hatua za utekelezaji sera ya
maji ya mwaka 2002 inayosisitiza ushirikishwaji wa watumia maji katika mipango
ya usimamizi wa rasilimali za maji.
Amesema kuwa kuundwa kwa jumuiya ya watumia
maji bonde dogo la mto Mfyamba ni hatua muhimu katika utekelezaji wa sera ya
maji. Ameutaka uongozi wa wilaya kuwa karibu na jumuiya hiyo katika utekelezaji
wa majukumu yake.
Akiongelea tatizo la kukauka kwa mto
Ruaha wakati wa kiangazi na kusababisha matatizo ya uzalishaji wa umeme katika
bwawa la Mtera na Kidatu, Afisa wa bonde la Rufiji amesema “hili ni tatizo la
kitaifa na tunastahili kulichukua hilimaanani kwani mto Mfyamba ni tawi la mto
Ndembera ambao ni tawi la muhimu la mto Ruaha Mkuu”. Amesema kutokana na hali
hiyo mchango wa wadau wote katika kuimarisha mtiririko wa maji katika mto Ruaha
mkuu ni wa muhimu sana na jamii mzima inastahili kuchukua hatua ili kuondoa
tatizo hilo. Amesema kuwa kukauka kwa mto wowote ni dalili ya matumizi mabaya
ya maji katika baadhi ya maeneo, ufanisi mdogo wa miundombinu ya umwagiliaji
katika maeneo hayo na uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji.
Bonde dogo la mto Mfyamba limeenea
katika wilaya za Mufindi na Mbarali.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni