Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Serikali imetoa rai kwa wawekezaji
zaidi kujitokeza katika uzalishaji wa mbegu bora ili kuinua kilimo na kukuza
uchumi nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri
wa Kilimo, Chakula na Ushirika Godfrey Zambi katika hotuba yake wakati wa hafla
fupi ya makabidhiano ya shamba la kuzalisha mbegu la Dabaga baina ya Wakala wa
kuzalisha mbegu na wakfu wa Clinton katika kijiji cha Lukani wilayani Kilolo.
Zambi amesema “tunaalika wawekezaji
wengi zaidi katika uwekezaji wa kilimo cha mbegu bora nchini”. Amesema kuwa
dhumuni kuu ni uzalishaji wa mbegu bora kwa kiwango kikubwa ili wananchi wengi
waweze kunufaika na upatikanaji wa mbegu bora nchini. Amesema kuwa serikali
inavutia uwekezaji katika kilimo cha uzalishaji wa mbegu kutokana na ukweli
kuwa uzalishaji wa mbegu nchini bado upo chini sambamba na matumizi ya mbegu
bora. Amesema kuwa katika kuhakikisha nchi inakuwa na mbegu bora na za kutosha
kwa ajili ya wakulima serikali inaendelea kujenga uwezo ikiwa ni pamoja na
kuishirikisha sekta binafsi.
Akiongelea faida wa shamba la
kuzalisha mbegu la Dabaga, naibu waziri amesema kuwa shamba hilo ni muhumu kwa
lengo la kupata mbegu kwa bei rahisi. Faifanyingine ameitaja kuwa ni
upatikanaji wa ajira ya moja kwa moja na ajira ya muda kwa wananchi na wakulima
wanaozunguka eneo la shamba hilo. Amesema kuwa wananchi watapata fursa ya
kujifunza juu ya uzalishaji wa mbegu bora katika shamba hilo.
Akiongelea majukumu ya wakala wa
kuzalisha mbegu nchini, Afisa mtendaji mkuu wa wakala wa kuzalisha mbegu nchini
Dkt. Firmin Mizambwa amesema kuwa wakala wanajukumu la kuongeza uzalishaji wa
mbegu bora kwa wakulima. Jukumu linguine amelitaja kuwa ni kuhamasisha ushiriki
wa sekta binafsi katika uzalishaji wa mbegu bora pamoja na kuongeza ajira kwa
wananchi wanaozunguka maeneo ya mashamba ya wakala hiyo. Amesema kuwa kutokana
na wakulima wengi kutotumia mbegu bora nchini, wakala wa mbegu unajukumu la
kuhamasisha matumizi ya mbegu bora nchini pamoja na kushirikiana na vituo vya
utafiti.
Katika salamu za kaimu katibu tawala
mkoa wa Iringa, Kilasi Mwakilasi amesema kuwa ushirikiano baina ya serikali na
sekta binafsi ni fursa muhimu kwa mkoa wa Iringa na wananchi wake. Amesema
ushirikiano huo unajikita katika maeneo mbalimbali yakiwa ni pamoja na
utaalamu, mafunzo na kuongeza fursa ya ajira.
Amesema kutokana na mkoa wa
Iringa kuwa mzalishaji mkubwa wa mahindi na alizeti ushirikiano huo utachangia
katika kukuza uzalishaji wa mazao hayo. Amesema kuwa mkoa wa Iringa utaendelea
kutoa ushirikiano kwa sekta binafsi kwa manufaa ya wananchi wa mkoa na taifa
kwa ujumla.
Shamba la kuzalisha mbegu bora la
Dabaga linaukubwa wa Hekta 1058.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni