TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA WACHANGIA DAMU DUNIANI
TAREHE 01 HADI 14 JUNI, 2014 ILIYOTOLEWA NA MKUU WA MKOA WA IRINGA OFISINI
KWAKE TAREHE 09/06/2014
Ndugu Wananchi,
Tanzania itaadhimisha kilele cha siku ya wachangia Damu duniani
tarehe 14 Juni, 2014 Kitaifa Mkoani Kigoma.
Ndugu Wananchi,
Kauli mbiu ya mwaka huu ambayo inaenda sambamba na miaka
11 tangu siku ya wachangia damu ilipoanzishwa ni “DAMU SALAMA UHAI WA MAMA” (SAFE
BLOOD FOR SAVING MOTHERS).
Ndugu
Wananchi,
Mkoa wa Iringa mwaka huu umebahatika kuwa mwenyeji wa Maadhimisho
ya Siku ya wachangia Damu duniani Kikanda kuanzia tarehe 1 Juni hadi tarehe 14
Juni, 2014 Siku ya Kilele itakayofanyika katika viwanja vya Mwembetogwa katika Manispaa
ya Iringa.
Ndugu
Wananchi,
Madhumuni ya siku hii ni kuongeza uelewa kwa
wananchi kuhusu umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari pia kuwatambua, kuwaenzi na
kuwashukuru wachangia damu ambao wamekuwa wakichangia damu kwa hiari mara kwa
mara bila malipo yoyote.
Ndugu
Wananchi,
Damu
ni uhai, hivyo kila binadamu mwenye ubinadamu na utu anayo nafasi ya kutoa damu
yake ambayo ni uhai kwa wahitaji wa tiba ya damu.
Ndugu Wananchi,
Vifo vingine vya akina mama katika
Hospitali zetu husababishwa na ukosefu wa damu iliyo salama. Hivyo kila mtu anaguswa
kwani hakuna asiyezaliwa na mama. Na ni
nani kama mama?
Ndugu Wananchi,
Kwanini kauli mbiu hii ya “uchangiaji
damu ni uhai wa mama” imetolewa mwaka huu?
Ukweli ni kwamba zaidi ya
asilimia 30 ya damu salama hutumiwa na akina mama wajawazito hasa wanapo pata
matatizo mbalimbali ya uzazi kama kutokwa na damu nyingi kabla au baada ya
kujifungua, mimba inapotoka au mama anapofanyiwa
upasuaji.
Ndugu Wananchi,
Damu ni uhai na ina thamani kubwa, Damu inaweza kuhifadhiwa kwa muda wa
siku 35 tu kabla ya muda wake wa kutumika kwisha. Hivyo zoezi la kuchangia damu
ni endelevu na la kudumu, chupa moja ya damu inaweza kuokoa maisha ya watu
zaidi ya mmoja kama ikigawanywa kitaalamu kwenye mazao mbalimbali za damu kama vile
plasma, chembe sahani na chembe nyekundu.
Ndugu Wananchi,
Huduma ya damu salama huokoa maisha ya
mamilioni ya watu kila mwaka duniani. Aidha, upatikanaji wa damu kwa wakati
huongeza nafasi ya kuishi kwa wahitaji wa damu,
Ndugu Wananchi,
Kwa kifupi nitayataja makundi ya watu ambao
huitaji damu na asilimia zake kama ifuatavyo:
·
Watoto
wadogo hasa walio chini ya umri wa miaka mitano (50%)
·
Wajawazito
na wanawake wenye matatizo ya uzazi (30%)
·
Majeruhi
wa ajali mbalimbali hasa ajali za barabarani na watu wanaofanyiwa tiba ya
upasuaji (15%)
·
Wale
wote wenye magonjwa mbalimbali yanayosababisha upungufu wa damu (5%)
Ndugu Wananchi,
Katika nchi yetu na kanda yetu mahitaji ya
damu yanazidi upatikanaji wake, Mpango wa Taifa wa Damu Salama unakabiliwa na
changamoto ya kuhakikisha kunakuwepo na upatikanaji wa damu salama na ya
kutosha ili kuweza kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji damu hospitalini.
Ndugu Wananchi,
Mahitaji ya damu Kitaifa ni wastani wa
chupa 400,000-450,000 Mpango wa Taifa wa Damu Salama unakusanya wastani wa
chupa 100,000-120,000 kwa mwaka.
Kikanda mahitaji ni wastani wa chupa za
damu 28,000 ambapo Kanda ya Nyanda za Kusini huweza kukusanya jumla ya chupa
19,331 ambayo ni sawa na asilimia 70 tu, hivyo tunakabiliwa na upungufu mkubwa
wa Damu Salama.
Ndugu Wananchi,
Uchangiaji damu wa hiari wa
bila malipo na wa mara kwa mara ni msingi wa upatikanaji wa damu salama na ya kutosha.
Wachangiaji damu wa kujirudia ni salama kwani damu yao ina kiasi kidogo cha
maambukizo ya magonjwa yanayoweza kuenezwa kwa njia ya damu.
Natoa rai kwa Wakazi wa Mkoa wa Iringa na Watanzania
wote kwa ujumla kujenga utamaduni wa kuchangia damu kwa hiari mara kwa mara ili
Kanda yetu iwe na akiba ya damu ya kutosha.
Ndugu Wananchi,
Iwapo asilimia moja ya Wakazi wa Kanda hii
wakiamua kuwa wachangiaji damu wa kujirudia Mpango wa Taifa wa Damu Salama
utaweza kukidhi mahitaji ya damu katika Hospitali zetu.
Ndugu Wananchi,
Damu Salama inatolewa bure katika vituo
vyote vya kutolea huduma kama mwananchi akiambiwa alipie damu atoe taarifa kwa
uongozi na ikibanika kweli mtumishi aliyefanya hivyo atachukuliwa hatua za
kinidhamu za kiutumishi.
Ndugu Wananchi,
Mkoa
wa Iringa umejiwekea mkakati wa kupunguza vifo vya uzazi na mtoto kupitia
mpango wa uwajibikaji katika kupunguza vifo hivyo na moja ya kipaumbele ni
uanzishwaji wa kituo kidogo cha kuchangia damu salama (Blood Collection
Satellite Site) Mkoani ambacho gharama yake ni Tshs. 140,000,000.00.
Hivyo,
nawaomba wadau na watu wote wenye mapenzi mema kuchangia kuanzishwa kwa kituo
hicho kurahisisha upatikanaji wa damu salama kwa wakati na kuokoa maisha ya
akina mama na watoto.
Ndugu Wananchi,
NAMALIZIA KWA KUSEMA NAWAOMBA WANANCHI MJITOKEZE KWA WINGI KATIKA SIKU HIZO
ZA MADHIMISHO ILI TUONYESHE MSHIKAMANO NA KUCHANGIA DAMU AMBAYO NI UHAI KWA MAMA.
KAULI MBIU: DAMU SALAMA UHAI WA
MAMA
ASANTENI
KWA KUNISIKILIZA
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni