Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkuu
wa mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma ameweka rekondi nyingine katika
mikesha ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2014.
Kauli
hiyo imetolewa na kiongozi wa wakimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa Rachel Kassanda
katika kijiji cha Idofi mkoani Njombe wakati akiwaaga wananchi wa mkoa wa
Iringa baada ya kukamilisha mbio hizo za siku nne mkoani Iringa.
Kassanda
amesema kuwa tokea Mwenge wa Uhuru umewashwa katika uwanja wa Kaitaba tarehe
2/5/2014 mkuu wa mkoa wa Iringa ameweza kushiriki katika mikesha mitatu
mfululizo. Amesema kuwa katika mikoa yote minane iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru
mwaka 2014, Dkt. Ishengoma ameonesha kitendo cha kipekee kilichopelekea hamasa
kwa wananchi kujitokeza na kushiriki katika mikesha ya Mwenge wa Uhuru. Amesema
kuwa kitendo hiki cha kizalengo hakina budi kuigwa ili kuongeza hamasa katika
mikesha ya Mwenge wa Uhuru.
Akiongelea
miradi ya maendeleo na thamani ya fedha katika miradi hiyo, Kassanda amesema
kuwa mkoa wa Iringa umeitendea haki miradi ya maendeleo ikilinganishwa na
thamani ya fedha iliyotumika. Amesema ushirikiano uliyopo baina na viongozi na
watendaji ni chachu katika kufanikisha miradi ya maendeleo kwa lengo la kutoa
huduma bora kwa wananchi.
Kiongozi
huyo wa wakimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa amewataka watumishi wa umma kusimama
katika nafasi zao kuhakikisha wanatenda haki na wajibu wao kwa wananchi na
serikali yao. Amesema kuwa mtumishi wa umma ni kioo cha wananchi na kuwataka
watumie nafasi wazopewa kuwahudumia wananchi kwa haki. Amesema kuwa sifa ya
mtumishi ni utoaji huduma kwa haki. Amewataka kuepuka vitendo vyote na
mazingira yanayotengeneza mianya ya rushwa. Amesema kuwa rushwa inafifisha haki
na kumfanya mwenye haki kudhulumiwa haki yake.
Kiongozi
wa wakimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa amesema kuwa kila mwaka mbio za Mwenge wa
Uhuru hubeba ujumbe maalum ambao unawajulisha na kuwatambulisha wananchi
masuala makuu yanayolikabili taifa kwa wakati huo. Amesema kuwa mbio za Mwenge
wa Uhuru mwaka 2014 zimebeba ujumbe usemao “Katiba ni sheria kuu ya nchi” wenye
kaulimbiu ‘jitokeze kupiga kura ya maoni tupate katiba mpya’. Amesema kuwa
ujumbe una lenga kuwahamasisha wananchi kujitokeza na kushiriki kupiga kura ya maoni ili kupata Katiba mpya
kwa mustakabali wa Taifa.
Iringa
ni mkoa wa tisa kutembelewa na Mwenge wa Uhuru mwaka 2014. Mikoa iliyotangulia
ni Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa, Mbeya, Singida, Dodoma na Morogoro. Ukitokea
Iringa mkoani Iringa Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika mkoa wa Njombe katika
halmashauri tano.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni