Frank Kibiki- KILOLO
VIKUNDI vya
wakulima wa zao la chai wilayani Kilolo, mkoani Iringa wamekabidhiwa matrekta
sita yenye thamani ya sh milioni 318 ili kusaidia kufufua kilimo chazao hilo
ambacho kimedorora katika wilaya hiyo.
Kukabidhiwa kwa
matrekta hayo kunawaletea tumaini jipya wakulima wa wilaya ya Kilolo, ambao
walianza kukata tamaa ya kulima zao hilo wakihofia soko.
Akikabidhi
matrekta hayo, Kiongozi wa mbio za Mwenge, Rahel Kassanda alisema kilimo cha
jembe la mkoni kimepitwa na wakati na kwamba, ili uzalishaji wa mazao wa kilimo
uongezeka ni lazima kutumia zana za kisasa.
Aliwataka
wakulima hao kutunza matrekta waliyokabidhiwa, ili yawasaidie katika kuendesha
kilimo cha kisasa ambacho kitawawezesha kuondokana na ugumu wa maisha.
Akisoma taarifa
ya wakulima hao, kaimu afisa kilimo wa wilaya ya Kilolo, Edward Mbembe alisema
mradi wa matrekta ulianza mwaka 2013 ukiwa na lengo la kuendeleza mnyololo wa
thamani wa zao la chai, kwa vikundi vya wakulima wadogo wa wilaya hiyo.
Alivitaja vikundi
vilivyokabidhiwa matrekta hayo kuwa ni Luhindo, Masisiwe, Mwatasi, Kidabaga,
Idete na Kimala.
Mbembe alisema
wakulima hao waliweza kuchangia sh milioni 78 huku halmashauri ya wilaya
kupitia mpango wa maendeleo ya kilimo, ilichangia sh milioni 240.
Wakizungumza na
uhuru, wakulima wa zao hilo walisema matrekta hayo yatawasaidia katika
kujikwamua kiuchumi kwa kuendesha kilimo cha kisasa ambacho, hawajawahi
kukilima.
Aidha waliiomba
serikali kujenga kiwanda cha chai wilayani humo ili iwe rahisi kwao kuuza raslimali
hiyo tofauti na sasa ambapo, watagemea viwanda vya wilaya nyingine.
Mwisho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni