Na. Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa - IRINGA
Mkoa wa Iringa
umejaaliwa fursa nyingi za uwekezaji ambazo zikitumika vizuri zitasaidia kuinua
pato la mwananchi na Taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo
imetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine
Ishengoma katika hotuba yake ya ufunguzi wa Baraza la Biashara la Mkoa wa
Iringa lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa VETA uliopo Manispaa ya
Iringa.
Baraza la Biashara la Mkoa wa Iringa |
Dkt. Ishengoma
amesema “Mkoa wa Iringa una fursa nyingi za uwekezaji kama tutazitumia vizuri
zinaweza kusaidia kukuza pato la mwananchi na Taifa kwa ujumla. Kuna fursa
katika utalii, viwanda, biashara, kilimo, kilimo cha maua, matunda, ufugaji,
misitu na huduma za jamii”. Amesema “ni jukumu letu sisi kuziainisha fursa hizi
na kufanya uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi”. Amesema kuwa Mkoa
wa Iringa ulishafungua milango kwa wawekezaji wa ndani na nje kuja kuwekeza.
Amesema kuwa Mkoa umejitahidi kuboresha mazingira na miundombinu ya uwekezaji
ila zoezi hilo linakabiliwa na changamoto ya kuzitangaza fursa hizo ili
zieleweke na kuvutia wawekezaji.
Dkt. Ishengoma
ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa amekitumia kikao hicho kuwapongeza
wawekezaji ambao wamekwisha zitambua fursa zilizopo za uwekezaji na kuzitumia
na kutoa wito kwa wawekezaji wengine kufuata mfano huo. Aidha, ameziagiza Halmashauri
za Mkoa wa Iringa kuwasaidia wawekezaji wanapojitokeza kuwekeza Iringa. Amezitaka
Halmashauri kuwa msaada kwa wawekezaji badala ya kuwa kikwazo. Amepongeza
juhudi za wawekezaji wanaowekeza katika hoteli za kitalii kwa lengo la kusaidia
kuinua sekta ya utalii mkoani Iringa.
Dkt. Ishengoma
amesema kuwa Taifa limeandaa mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini
awamu ya pili (2011-2015) unaolenga kufikia Dira ya Taifa ya maendeleo ya mwaka
2025. Amesema kuwa mkukuta umejengwa katika nguzo tatu na kuzitaja kuwa ni
kuhamasisha ubora wa maisha ya watu na ustawi wa jamii. Nguzo nyingine ni
ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini wa kipato na utawala bora na
uwajibikaji. Amesema kuwa kufanikiwa kwa malengo ya mkukuta kunategemea
ushiriki wa wadau wote katika utekelezaji wake.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni