Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-IRINGA
Mazingira mazuri ya uwekezaji ni
jambo lililochangia kuvutia wawekezaji mitaji nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Uwekezaji na Uwezeshaji Dkt. Mary Nagu alipokuwa
akimkaribisha Waziri Mkuu kufungua kongamano la uwekezaji kwa mikoa ya Iringa,
Njombe na Mbeya lililofanyika jijini Mbeya.
Dkt. Nagu amesema kuwa mazingira
mazuri ya uwekezaji nchini Tanzania yamewezesha kuvutia wawekezaji mitaji.
Amesema Tanzania imevutia mitaji mingi zaidi hadi kufikia mwaka 2013 dola za
kimarekani shilingi Bilioni 1.87 zaidi katika sekta ya utafutaji madini,nishati
na gesi.
Akiongelea uwezeshaji wa ndani,
Waziri wa Nchi OWM-UU amesema kuwa uwekezaji wa ndani ni jambo muhimu katika
ukuzaji wa uchumi nchini. Amesema kuwa uwekezaji wa ndani ni muhimu kwa sababu
faida kubwa inabaki ndani ya nchini. Aidha, ametoa wito kuhakikisha kila
uwekezaji unamletea mwananchi mafanikio yanayoonekana na si mafanikio ya
kihisia.
Waziri Dkt. Nagu amesema kuwa kongamano ni
muhimu na litakisaidia kituo cha uwekezaji nchini (TIC) kuainisha fursa za
uwekezaji zilizopo kwa lengo la kuvutia uwekezaji zaidi. Amesema kuwa kongamano
hilo litasaidia kuandaa takwimu sahihi za miradi inayohitaji uwekezaji katika ukanda
wa Nyanda za Juu Kusini. Aidha, amewashauri wawekezaji wa ndani kukitumia
ipasavyo kituo cha Taifa cha uwekezaji ili waweze kunufaika na shughuli za
kituo hicho. Amesema kuwa TIC ikitumika ipasavyo kutapunguza na kuepuka
matapeli wanaojichomeka kwa jina la kuto hicho cha uwekezaji kwa lengo la
kujinufaisha.
Dkt. Nagu ameutaja ukanda wa kusini
kuwa ni ukanda wenye rasilimaji nyingi kuliko kanda zote na kuwataka wawekezaji
kutumia fursa ya rasilimali hiyo kujiletea maendeleo.
Waziri Dkt. Nagu amezitaja changamoto
zinazoikabili mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya kuwa ni usafiri hasa wa reli na
barabara. Amesema kuwa serikali imeanza kukabiliana na changamoto hizo kwa
kuimarisha miundombinu ya reli na barabara ili kuzifanya changamoto hizo kuwa
historia.
Kongamano hili ni muendelezo wa utaratibu
uliowekwa kuweza kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo na ambazo
hazijavumbuliwa.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni