Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa- IRINGA
Wadau wa masuala ya kilimo
wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wametakiwa kubuni mkakati wa kijitangaza ili
shughuli zao hazifahamiki kwa watu wengi zaidi.
Kauli hiyo imetolewa na
mgeni rasmi wakati wa kukagua mabanda ya maonesho Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt.
Christine Ishengoma wakati wa majumuisho baada ya kutembelea mabanda ya
maonesho ya Nanenane katika uwanja wa maonesho wa John Mwakangale jijini Mbeya.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, dkt. Christine Ishengoma (Mb.) kushoto na mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Nuhu Mwasumilwe (kulia) |
Dkt. Ishengoma amesema
kuwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini imepiga hatua kubwa sana katika matumizi ya
teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) lakini shughuli hizo hazitangazwi.
Amesema kuwa vyuo vikuu vinafanya kazi nzuri katika matumizi ya Tehama katika
kubuni na kutengeneza nafasi za kazi. Amesema kuwa ubunifu huo ni mzuri hasa
katika kuwasaidia vijana kujiajiri na kupunguza tatizo la ajira kwa vijana
nchini. Amesema kuwa teknolojia zinazobuniwa na vyuo vikuu zitangazwe na
kusambazwa kwa mujibu wa taratibu.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa
amewataka wakazi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kujikita katika kilimo cha
mbogamboga, matunda na maua. Ameshauri matumizi ya “greenhouse” kwa sababu
mkulima anaweza kulima kilimo cha mbogamboga na matunda katika eneo dogo kwa
ufanisi na tija kubwa. Aidha, amewashauri wananchi kutengeneza na kutumia
teknolojia ya “greenhouse” katika maeneo yao ili iweze kuwasaidia katika
kujipatia mahitaji ya mbogamboga na matunda. Amesema kuwa kufanya hivyo
kutawahakikishia uhakika wa mbogamboga na matunda kwa familia na kuuza kwa watu
wengine na kujiongezea kipato.
Wakati huohuo, Mwakilishi
wa Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Nuhu Mwasumilwe katika ukaguzi wa mabanda
amepongeza jitihada za hospitali ya rufaa ya Mbeya kununua mashine ya kusafisha
figo. Amesema kuwa ununzi wa mashine hiyo utasaidia wananchi wengi wanaosumbuliwa
na tatizo la figo. Amesema kuwa mashine hiyo itasaidia kupunguza muda wa
wananchi kutumia kufuata huduma hiyo na badala yake kujihusisha na shughuli za
kilimo.
Nuhu Mwasumilwe |
Mwasumilwe ambaye pia ni
Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Mipango na Uratibu katika Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Iringa amepongeza ufugaji wa nyuki katika Wilaya ya Mufindi ambapo
mfugaji Bahati Mhapa amekuwa akifuga nyuki kwa tija. Amesema kuwa mfugaji huyo
mwenye mizinga zaidi ya 800 amekuwa
akizalisha zaidi ya tani 2.5 za asali kwa mwaka. Amesema kuwa changamoto kubwa
ni uhitaji wa soko la nje ambalo ni kubwa sana kuliko uwezo wa kuzalisha asali
hapa nchini. Mwasumilwe ametoa wito kwa wananchi kuwekeza katika ufugaji wa
nyuki kwa kiwango kikubwa ili kunufaika na soko la nje.
Akiongelea udanganyifu wa
kuuza mbegu, Mwasumilwe amekemea tabia ya udanganyifu kwa baadhi ya
wafanyabiashara wanaouza mbegu feki. Amesema kuwa ni vizuri wauzaji wa mbegu
wakatambuliwa ili kukabiliana na wauzaji feki wa mbegu nchini.
Akiwasilisha tathmini yake
alipotembelea mabanda mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Grace Macha
ametoa rai kwa wananchi kutumia teknolojia ya kufua umeme inayotengenezwa na
chuo cha ufundi stadi VETA. Amesema kwa kutumia teknolojia hiyo rahisi
kutasaidia kaya masikini kuwa na nishati ya umeme kwa gharama nafuu.
Grace Macha |
Macha ambae pia ni Afisa
Kilimo Mkuu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa amewataka wananchi hasa
wakulima kutumia taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini katika
shughuli za kilimo. Amesema kuwa zipo taarifa nyingi muhimu zinazotolewa na Mamlaka
hiyo zinazoweza kuwasaidia wakulima lakini haziwafikii wakulima kutokana na
kutokuwa na utaratibu muafaka wa kuziunganisha taarifa hizo na wakulima.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni