Ijumaa, 8 Agosti 2014

MAZIWA YA MAMA NI KINGA DHIDI YA MARADHI



Na. ofisi ya Mkuu wa Mkoa IRINGA
Maziwa ya mama yanatosha kujenga mwili wa mtoto na kuupa nguvu za kukabiliana na maradhi pasipo kutumia chakula kingine chochote kwa miezi sita ya mwanzo.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Charles Pallangyo  aliyekuwa ngeni rasmi kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji duniani yaliyofanyika mjini Mafinga wilayani Mufindi.
Katibu Mkuu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Charles Palangyo
Palangyo amesema “maziwa ya mama yanatosha kujenga mwili wake, kuupa nguvu na kuukinga dhidi ya maradhi. Umri sahihi wa kumwanzishia mtoto vyakula vya nyongeza, maji au vinywaji vingine vya ziada ni wakati anapotimiza umri wa miezi sita”. Amesema kuwa mtoto anapaswa kuendelea kunyonyeshwa hadi afikishe umri wa miaka miwili au zaidi na kusisitiza kuwa kipindi hicho maziwa ya mama huendelea kuchangia mahitaji ya mtoto kilishe.   
Katibu Mkuu amesema kuwa watoto wanaonyonyeshwa vizuri huwa na maendeleo mazuri katika ukuaji wao kimwili na kiakili jambo linalowafanya kuwa na uelewa mkubwa wa mambo. Amesema kuwa kunyonya vizuri kusawasaidia kufanya vizuri shuleni kwa kupata alama mzuri darasani. Amesema kuwa kunyonya vizuri maziwa hayo huwafanya watoto kuwa na uwiano mzuri wa uzito na urefu na kuepusha tatizo la ukondefu. Amesema kuwa maziwa hayo huwasaidia kuwa na uwiano mzuri wa uzito na umri jambo linatoondoa tatizo la uzito mdogo.
Akiongelea athari za kutokunyonyesha watoto maziwa ya mama, Palangyo amezitaja athari hizo kuwa ni kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaopata maradhi ya kuhara, mfumo wa kupumua na watoto kuwa na uzito uliozidi na kiribatumbo ambayo huweza kuwaletea maradhi yasiyo ya kuambukiza kama moyo.
Katika salamu za mkuu wa mkoa wa Iringa zilizosomwa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu amesema kuwa katika kukabiliana na tatizo la utapiamlo mkali mkoani Iringa, serikali kupitia wizara ya afya na ustawi wa jamii imeanzisha progrmu ya kuongeza virutubishi kwenye chakula hasa unga wa ngano, mahindi na mafuta ya kula. Amesema kuwa programu hiyo itboresha afya za watanzania hasa wanawake wajawazito na kuwapatia virutubisho vya kutosha kulisha watoto wachanga wakiwa tangu tumboni kwa mama zao na baada ya kujifungua kupitia maziwa ya mama.
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu
Akiongelea takwimu, Wamoja amesema kuwa takwimu za kiafya na kidemografia zinaonesha kuwa asilimia 52 ya watoto chini ya miaka mitano wana udumavu katika mkoa wa Iringa ikilinganishwa na kitaifa asilimia 42. Amesema kuwa upande wa wanawake walio kwenye umri wa kujifungua takwimu zinaonesha kuwa kuwa asilimia 10.9 ya wanawake wajawazito wana maambukizi ya Ukimwi ikilinganishwa na wastani wa kitaifa ambao ni asilimia 5.7 kwa takwimu za viashiria vya Malaria na Ukimwi za mwaka 2012.
=30= 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...