Jumatatu, 8 Septemba 2014

KAMPENI YA CHANJO YA SURUA KUANZA SEPTEMBA 24-30 NCHINI


Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa IRINGA
Serikali imedhamiria kutokomeza ugonjwa wa Surua kwa kufanya kampeni ya kitaifa ya chanjo ya Surua-Rubella kwa watoto wote wenye umri usiozidi miaka 14.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Dkt. Leticia Warioba

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Dkt. Leticia Warioba katika ufunguzi wa kikao cha kamati ya uraghabishi na uhamasishaji wa kampeni ya chanjo ya Surua-Rubella ya Mkoa wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Dkt. Ishengoma amesema kuwa kuanzia mwaka 1999 serikali imekuwa ikifanya kampeni za chanjo ya surua kila baada ya miaka mitatu. Amesema kuwa kabla ya kuanza kampeni hiyo mwaka 1999 takwimu zilionesha kuwa karibu asilimia 90 ya watoto walio chini ya miaka 15 walipata ugonjwa wa surua. Amesema kuwa zaidi ya watoto milioni mbili kati yao walifariki na kati ya watoto 15,000 na 60,000 walipata ulemavu wa kutoona kila mwaka duniani. Amesema kuwa maradhi haya yanapungua kwa sababu ya kuimarishwa utoaji wa chanjo kwa watoto kwa zaidi ya asilimia 80.

Mkuu wa Mkoa amesema kuwa kuanzia tarehe 24 hadi 30 Septemba, 2014 Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo ikishirikiana na wadau wa chanjo itafanya kampeni ya kitaifa ya Chanjo ya Surua-Rubella kwa watoto wote walio na umri kati ya miezi tisa hadi miaka 14. Amesema kuwa kampeni  hiyo itahusisha utoaji wa matone ya chanjo ya kuzuia kupooza kwa watoto wenye umri wa miezi 0 hadi miezi 59, utoaji wa vidonge vya  vitamin 'A' kwa watoto wenye umri wa miezi 6 hadi miezi 59 na vidonge vya kutibu minyoo kwa watoto wenye umri wa miezi 12 hadi 59. 
Wadau wa Chanjo Mkoa wa Iringa

Wadau wa chanjo Mkoa wa Iringa

Akiongelea kampeni hiyo mkoani Iringa, Mkuu wa Mkoa amesema kuwa kampeni hiyo itahusisha watoa chanjo 548, wahamasishaji 822 ikitarajia kuwafikia watoto 429,078 wenye umri wa miezi 9-14. Amesema kuwa chanjo ya Surua-Rubella inaanzishwa nchini kwa ushauri wa kitaalamu wa Shirika la Afya duniani.

Amesema kuwa pamoja na kiwango cha chanjo kuwa juu bado milipuko imeendelea kutokea kutokana na karibu asilimia 20 ya watoto ambao hawakupata chanjo hiyo awali na wa le waliopata chanjo kwenye umri wa miezi 9 karibu asilimia 15 hawakupata kinga kwa sababu za kibaiojia katika umri huo.
=30=

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...