Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa IRINGA
Maandalizi ya mtihani wa kumaliza Elimu
ya Msingi mwaka 2014 mkoani Iringa yamekamilika na jumla ya wanafunzi 21,540
wanatarajiwa kufanya mtihani huo.
Mwl. Joseph Mnyikambi |
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala
Msaidizi, Sehemu ya Elimu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mwl. Joseph
Mnyikambi alipokuwa akiongea na waandishi wa Habari kuhusu maandalizi ya
mtihani huo utakaoanza tarehe 10-11/9/2014 kwa mkoa wa Iringa ofisini kwake.
Mwl. Mnyikambi amesema “jumla ya
wanafunzi 21,540 (wavulana 9,779 na wasichana 11,761) ndiyo watafanya mtihani
wa kumaliza Elimu ya Msingi mwaka 2014”. Amesema kuwa idadi ya wanafunzi
watakaofanya mtihani huo imepungua ikilinganishwa na mwaka 2013 ambapo kulikuwa
na watahiniwa 23,149 (wavulana 10,753 na wasichana 12,396) waliosajiliwa.
Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Elimu
amesema kuwa maandalizi yote yamekamilika na vifaa vyote vinavyohusiana na
mtihani huo tayari vimepelekwa kwenye Halmashauri zote za Mkoa wa Iringa.
Aidha, ametoa wito kwa wazazi wenye
watoto wanaosoma darasa la saba kuhakikisha watoto wao wanakwenda kufanya
mtihani huo. Amewataka wanafunzi wote wa darasa la saba kuzingatia maelekezo
watakayopewa na wasimamizi.
Waandishi wa Habari |
Waandishi wa Habari |
Mkoa wa Iringa una jumla ya shule za
msingi 484 kati ya shule hizo shule 458 ndizo zenye wanafunzi watakaofanya
Mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi mwaka 2014.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni