Jumatatu, 15 Desemba 2014

WADAU WA MAJI WATAKIWA KUFUNGUKA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wadau wa sekta ya maji wilaya za Iringa na Mufindi wametakiwa kufuatilia kwa umakini na kutoa maoni kwa lengo la kuboresha taarifa ya mtaalamu mshauri ya kazi ya tathmini ya athari za kijamii na kimazingira kuhusu ujenzi wa bwawa la Lugoda kwenye mto Ndembera wilayani Mufindi.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa wilaya ya Iringa, Dkt. Leticia Warioba katika mkutano wa wadau kujadili taarifa ya kazi ya tathmini ya athari za kijamii na kimazingira ya ujenzi wa bwawa la Lugoda kwenye mto Ndembera.


Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Dkt. Leticia Warioba
Masenza amesema “kutokana na umuhimu wa ujenzi wa bwawa katika mto Ndembera kwa jamii yetu, napenda kuwashauri muwe wasikivu ili muweze kutoa maoni yenu ambayo yataisaidia pia serikali kufanya maamuzi ya hatua zitakazofuata. Nia yetu sote iwe ni kujenga kwa kuboresha taarifa itakayowasilishwa ili iweze kukidhi matarajio yetu kama wadau na wananchi wetu juu ya umuhimu wa ujenzi wa bwawa la Lugoda katika mto Ndembera”.
Amesema kuwa Wizara ya Maji kupitia ofisi za Maji Bonde la Rufiji inatekeleza mradi wa ujenzi wa bwawa la Lugoda katika mto Ndembera likiwa ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kitaifa inayotekelezwa kupitia programu ya uendelezaji wa sekta ya Maji (WSDP). Amesema kuwa ili kuweza kutekeleza mradi huo ilikuwa ni muhimu kwanza kufanya tathmini ya athari za kimazingira na kijamii.  “Kutokana na hali hiyo, kikao hiki kitapokea taarifa iliyoandaliwa na mtaalam mshauri na kuijadili kwa kina, kisha kutoa maoni ambayo yatasaidia kuiboresha” alisisitiza Mkuu wa Mkoa.
Katika maelezo ya utangulizi yaliyotolewa na Afisa Maji wa Bonde la Rufiji Idris Msuya amesema kuwa Wizara ya Maji kwa kushirikiana na bodi ya Bonde la Rufiji kupitia mfuko wa programu ya sekta ya maendeleo ya Maji ina mpango wa kujenga bwawa katika kijiji cha Lugoda Lutali kilichopo wilayani Mufindi kwenye mto Ndembera. Amesema kuwa lengo la ujenzi huo ni kuhifadhi maji ili kupata mtiririko endelevu kwenye mto Ruaha mkuu katika kipindi cha kiangazi kwa ajili ya matumizi ya binadamu na mazingira. Aidha, amesema kuwa lengo jingine ni kuzalisha umeme kwenye maporomoko ya Maluluma yaliyopo katika kijiji cha Igomaa.
Afisa Maji wa Bonde la Rufiji, Idris Msuya
Ameyataja malengo mengine kuwa ni kuanzisha shughuli za kilimo cha umwagiliaji kwenye eneo la mradi, uvuvi na shughuli za utalii.
=30=

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...