Na. Ofisi ya Mkuu
wa Mkoa
Wadau
wa sekta ya maji wilaya za Iringa na Mufindi wametakiwa kufuatilia kwa umakini
na kutoa maoni kwa lengo la kuboresha taarifa ya mtaalamu mshauri ya kazi ya
tathmini ya athari za kijamii na kimazingira kuhusu ujenzi wa bwawa la Lugoda
kwenye mto Ndembera wilayani Mufindi.
Rai
hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba
iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa wilaya ya Iringa, Dkt. Leticia Warioba
katika mkutano wa wadau kujadili taarifa ya kazi ya tathmini ya athari za
kijamii na kimazingira ya ujenzi wa bwawa la Lugoda kwenye mto Ndembera.
Masenza
amesema “kutokana na umuhimu wa ujenzi wa bwawa katika mto Ndembera kwa jamii
yetu, napenda kuwashauri muwe wasikivu ili muweze kutoa maoni yenu ambayo
yataisaidia pia serikali kufanya maamuzi ya hatua zitakazofuata. Nia yetu sote
iwe ni kujenga kwa kuboresha taarifa itakayowasilishwa ili iweze kukidhi
matarajio yetu kama wadau na wananchi wetu juu ya umuhimu wa ujenzi wa bwawa la
Lugoda katika mto Ndembera”.
Amesema
kuwa Wizara ya Maji kupitia ofisi za Maji Bonde la Rufiji inatekeleza mradi wa
ujenzi wa bwawa la Lugoda katika mto Ndembera likiwa ni miongoni mwa miradi
mikubwa ya kitaifa inayotekelezwa kupitia programu ya uendelezaji wa sekta ya Maji
(WSDP). Amesema kuwa ili kuweza kutekeleza mradi huo ilikuwa ni muhimu kwanza
kufanya tathmini ya athari za kimazingira na kijamii. “Kutokana na hali hiyo, kikao hiki kitapokea
taarifa iliyoandaliwa na mtaalam mshauri na kuijadili kwa kina, kisha kutoa
maoni ambayo yatasaidia kuiboresha” alisisitiza Mkuu wa Mkoa.
Katika
maelezo ya utangulizi yaliyotolewa na Afisa Maji wa Bonde la Rufiji Idris Msuya
amesema kuwa Wizara ya Maji kwa kushirikiana na bodi ya Bonde la Rufiji kupitia
mfuko wa programu ya sekta ya maendeleo ya Maji ina mpango wa kujenga bwawa
katika kijiji cha Lugoda Lutali kilichopo wilayani Mufindi kwenye mto Ndembera.
Amesema kuwa lengo la ujenzi huo ni kuhifadhi maji ili kupata mtiririko
endelevu kwenye mto Ruaha mkuu katika kipindi cha kiangazi kwa ajili ya
matumizi ya binadamu na mazingira. Aidha, amesema kuwa lengo jingine ni
kuzalisha umeme kwenye maporomoko ya Maluluma yaliyopo katika kijiji cha
Igomaa.
Ameyataja
malengo mengine kuwa ni kuanzisha shughuli za kilimo cha umwagiliaji kwenye
eneo la mradi, uvuvi na shughuli za utalii.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni