Alhamisi, 19 Februari 2015

IRINGA YAJITOSHELEZA KWA CHAKULA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkoa wa Iringa unajitosheleza kwa chakula ukiwa na ziada ya tani 1,032,613 kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2013/2014.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Amina Masenza alipokuwa akiwasilisha taarifa ya Mkoa wa Iringa kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayeendelea na ziara ya kikazi Mkoani Iringa.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe Amina Masenza
Amesema katika msimu wa kilimo wa mwaka 2013/2014 Mkoa wa Iringa ulipata mavuno jumla ya tani 1,379,602 kwa mazao ya nafaka na mikunde.
Amesema kulingana na tathmini iliyofanyika mwezi Septemba, 2014 kuhusu mavuno yaliyopatikana, Mkoa unajitosheleza kwa chakula na kuwa na ziada ya tani 1,032,613 ikilinganishwa na mahitaji ya Mkoa ya tani 346,989. Amesema katika msimu wa mwaka 2014/2015 Mkoa umelenga kulima hekta 527,281 za mazao ya chakula ambazo zinatarajia kuzalisha tani 1,499,016.
Kuhusu utekelezaji wa malengo ya kilimo, Mkuu wa Mkoa amesema kuwa Mkoa umekuwa ukifanya vizuri katika sekta ya kilimo na kupata mafanikio mengi.
Ameyataja mafanikio hayo kuwa ni kuongeza eneo linalolimwa mazao ya chakula kutoka hekta 365,650 msimu wa mwaka 2010/2011 hadi kufikia hekta 577,235 msimu wa mwaka 2014, sawa na ongezeko la asilimia 58. Mkoa una eneo linaloweza kumwagiliwa lenye jumla ya hekta 54,446, kati ya hekta hizo, zinazomwagiliwa kwa sasa ni hekta 25,585 sawa na asilimia 47 ya eneo lote. Uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani 693,927 kwa msimu wa mwaka 2010/2011 hadi kufikia tani 1,379,602 msimu wa mwaka 2013/2014 sawa na ongezeko la asilimia 98.8.
Mkoa wa Iringa unategemea kilimo ikiwa zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wake hujihusisha na shughuli za kilimo.
=30=



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...