Na. Namsembeli Mduma, Habari Leo
Wanafunzi
wa shule za serikali za kata zinazobezwa kwa kuitwa yeboyebo wametakiwa
kuendelea kufanya vizuri waitoe kimasomaso serikali isikashifiwe kwa jitihada
zake za kuendeleza shule hizo.
Akizungumza
kwenye Ikulu ndogo mjini hapa juzi, waziri Mkuu, mizengo panda ambaye yuko
kwenye ziara ya kikazi mkoani humu, alisema kilichofanywa na wanafunzi wa shule
ya sekondari Igowole ya Mufindi ni ishara kuwa shule hizo zinaweza kuwa vinara
wa ufaulu, tofauti na inavyofikiriwa.
Kwa
mujibu wa panda, kumekuwa na mitazamo hasi miongoni mwa baadhi ya watu kuhusu
shule za serikali za kata, kiasi cha kuwafanya wanaosoma katika shule hizo kukata
tama wakiamini kuwa hawawezi kufaulu wakisoma kwenye shule hizo.
Hata
hivyo rekodi ya matokeo ya mtihani wa kidato cha sita mwaka 2013, kama
ilivyotolewa kwa waziri mkuu na mkuu wa mkoa huo, Amina Masenza zinaonesha kuwa
mkoa ulifanya vizuri katika mtihani huo, ambapo asilimia 99 ya watahiniwa wote
walifaulu.
Kutokana
na rekodi hizo, shule ya sekondari Igowole ambayo ni ya serikali ya Kata
iliongoza kitaifa, huku shule nyingine ya sekondari iitwayo Kawawa ambayo pia
ipo katika wilaya ya Mufindi ilikuwa katika 10 bora kitaifa.
“ninawapongeza
viongozi, walimu na wanafunzi kwa bidii mnayoionesha. Mnaitwa yeboyebo kuonesha
kuwa hamuwezi, lakini cha kufurahisha ni kwamba, pamoja na changamoto nyingi
mnaweza tena zaidi ya wanaomini kuwa ndio wenyewe katika masuala haya ya
elimu,” alisema na kuwaomba waendeleze bidii hiyo ili serikali itoke
kimasomaso.
Wakati
huohuo, Masenza alimweleza waziri mkuu kuwa ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha
nne umeongezeka kutoka asilimia 52.1 mwaka 2010 hadi asilimia 65.2 mwaka 2013,
jambo linalofanya mkoa huo uzidi kupata moyo wa kutukumia mbinu bora zaidi za
ufundishaji kupanua uelewa.
Alitaja
mafanikio mengine katika eneo la elimu kuwa ni pamoja na kufaulu kwa wanafunzi
14,650 wa darasa la saba mwaka jana, ambao ni kati ya wanafunzi 21,363, sawa na
asilimia 68.5
“mwaka
2010 wanafunzi 24,035 walifanya mtihani wa darasa la saba ambapo 15,512 sawa na
asilimia 64.5 walifaulu vizuri,” Masenza alisema.
Waziri
Mkuu alisema, serikali inatambua changamoto zilizopo katika sekta ya Elimu na
kuzitafutia ufumbuzi wa kina.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni