Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Waziri
Mkuu amepongeza ujenzi wa Maabara katika shule ya sekondari ya Kihesa kuwa imedhihirisha
thamani halisi ya fedha.
Kauli
hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Pinda
alipokagua maendeleo ya ujenzi wa Maabara katika shule hiyo.
“Kihesa
sekondari Maabara imejengwa haikukarabatiwa” alisema Mhe. Pinda. Kauli hiyo
imekuja kufuatia baadhi ya maeneo kukarabati Maabara za zamani badala ya
kujenga Maabara mpya. Amesema kuwa agizo la Mhe. Rais lilikuwa ni kujenga Maabara
si kukarabati zilizopo. Aidha, ameoneshwa kusikitishwa na baadhi ya maeneo
kubadilisha vyumba vya Madarasa kuwa Maabara. Amesema utaratibu huo unaondoa
dhana ya ujenzi wa Maabara kwa sababu vyumba hivyo ni vidogo ikilinganishwa na
vipimo halisi vya ramani ya sasa ya Maabara. Amesema kuwa mabadiliko hayo ya
vyumba vya Madarasa kuwa Maabara kutasababisha upungufu wa vyumba vya Madarasa.
Akiongelea
suala la nidhamu kwa wanafunzi, Waziri Mkuu amewapongeza walimu na wazazi kwa
kusimamia nidhamu ya wanafunzi katika shule hiyo. Pongezi hizo zimetokana na
tathmini ya haraka iliyofanywa na Mhe. Pinda katika shule hiyo juu ya mavazi ya
wanafunzi. Amesema kuwa nidhamu inahusisha mavazi pia. Amesema sehemu nyingine
alizotembelea amewakuta wanafunzi wavulana wamevaa suruali katikati ya makalio.
Wakati
huohuo, mke wa Waziri Mkuu mama Tunu Pinda amechukua fursa hiyo kuwatakia heri
wanafunzi wa shule ya sekondari kihesa. Amewataka wanafunzi hao kuwa ‘wasongolist’
akimaanisha kuwa wawe wanaopenda kujisomea zaidi ya mambo mengine ili kuongeza
ufaulu wao. Amewataka kuendeleza nidhamu katika mavazi ili waendelee
kuheshimika katika jamii inayowazunguka.
Waziri
Mkuu yupo katika ziara ya kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo katika Mkoa
wa Iringa akiwa katika siku yake ya tano amefanya ziara katika Manispaa ya
Iringa kwa kukagua maendeleo ya ujenzi wa Maabara pamoja na mambo mengine.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni