Na. Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa
Wilaya ya Kilolo imeshauriwa kuunda Halmashauri mbili ili
kuwarahisishia na kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda alipokagua
skimu ya umwagiliaji ya Nyanzwa iliyopo Wilayani Kilolo.
Mhe. Pinda amesema “kwa kuzingatia hali halisi ya jiografia ya
Wilaya ya Kilolo ambayo ina wakazi wanaoishi milimani na wengine wanaishi
mabondeni, nashauri uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo na uongozi wa
Mkoa ukae pamoja na kuangalia uwezekano wa kuanzisha Halmashauri mbili (2).
Halmashauri moja ishughulikie maendeleo ya wananchi wanaoishi milimani na
Halmashauri ya pili ishughulie maendeleo ya wananchi wanaoishi mabondeni kwa
kuwa mazingira yao ni tofauti.” Amesema kuwa hatua hiyo itasogeza huduma za
maendeleo karibu na wananchi tofauti na hali ilivyo sasa. Ameutaka uongozi wa Mkoa
kuwasilisha mapema maombi hayo Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI.
Aidha, ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Kilolo kutazama upya
ukubwa wa maeneo ya utawala ya Kata zake na kuzigawanya kwa kuwa kwa sasa
maeneo ni makubwa sana jambo ambalo linasababisha wananchi kukosa huduma za
muhimu karibu.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni