Na. Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa
Halmashauri ya Manispaa ya Iringa umetakiwa kufanya mapitio ya
Mpango wa Mji kwa kushirikisha wataalam wa Chuo kikuu cha Ardhi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda alipokuwa
akiongea na wananchi wa Manispaa ya Iringa katika uwanja wa shule ya msingi
Ipogolo iliyopo katika Manispaa ya Iringa.
Mhe. Pinda amesema kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ina
historia ndefu kwa kuwa ilitangazwa kuwa Mji mwaka 1955 na kuwa Manispaa mwaka
1988. Manispaa ya Iringa ina Kata 18 na Mitaa 192 na Wakazi 150,000. Amesema
kuwa changamoto yake kubwa ni kuwa na eneo dogo la Kilometa za Mraba 331 tu,
sawa na takriban asilimia moja ya eneo la Mkoa ambalo ni Kilometa za Mraba
35,700.
”Nashauri uongozi wa Manispaa ya Iringa mfanye mapitio ya Mpango
wa Mji wa Manispaa ya Iringa (Master Plan) kwa kushirikiana na Wataalam kutoka
Chuo Kikuu cha Ardhi ili Mji wenu upangwe vizuri zaidi na mpime viwanja kwa
utalaam wa kisasa” alisema Mhe. Pinda.
Ameitaka Halmashauri hiyo kujitahidi kuwa mbele ya wananchi kwa
kupima viwanja ili kuepuka wananchi kujijengea makazi yao kiholela halafu
baadaye wanawabomolea nyumba zao nzuri. Amewakata lengo lao liwe kuwawezesha wananchi
kujenga nyumba bora katika maeneo yaliyopimwa viwanja. Waziri Mkuu alitumia mkutano
huo kuziagiza Halmashauri zote nchini ziimarishe Idara za Mipango Miji na
zikope kwa ajili ya kupima viwanja.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni