Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkoa wa Iringa umeendelea kufanya
vizuri katika ufaulu wa mitihani ya elimu ya msingi kwa zaidi ya miaka 15
mfululizo.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Michezo
Mkoa wa Iringa, Bw. Kenneth Komba alipowasilisha taarifa ya sekta ya elimu kwa
niaba ya Afisa Elimu Mkoa wa Iringa katika kikao baina ya viongozi wa Mkoa na
viongozi wa dini kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa
mkoa wa Iringa.
Bw. Komba amesema “mkoa umeendelea
kushika nafasi ya tatu na nne kitaifa katika ufaulu kwenye mtihani wa kuhitimu
elimu ya msingi kwa kipindi cha miaka 16 mfululizo”. Amesema kuwa mwaka 2014
shule za kwanza na kumi kitaifa katika mtihani wa kidato cha sita zilitoka
katika mkoa wa Iringa. Amezitaja shule hizo za sekondari kuwa ni Igowole
iliyoshika nafasi ya kwanza na Kawawa iliyoshika nafasi ya 10.
Akiongelea uandikishaji wanafunzi wa
madarasa ya awali na msingi, Afisa Michezo amesema kuwa uandikishaji huo
unaendelea kwa zaidi ya asilimia 99 kwa kila halmashauri za mkoa wa Iringa.
Akiongelea changamoto zinazoikabili
sekta ya elimu mkoani Iringa, Bw. Komba ameitaja changamoto kubwa kuwa ni
upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi kwa shule za sekondari. Changamoto
nyingine ameitaja kuwa ni madeni makubwa ya chakula kwa shule za bweni.
Mkoa wa Iringa una jumla ya shule za
msingi 487 na shule 160 zikiwa ni za sekondari.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni