Ijumaa, 15 Mei 2015

RC MASENZA AOMBA USHIRIKIANO NA VIONGOZI WA DINI IRINGA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Viongozi wa dini mkoani Iringa wametakiwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali kuhakikisha maisha bora kwa wananchi yanawezekana.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bibi. Amina Masenza alipokuwa akiongea na viongozi wa dini katika kikao maalumu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bibi. Amina Masenza (kulia)
Bibi. Masenza amesema kuwa viongozi wa dini ni muhimu sana katika kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali na kufikisha ujumbe kwa watu wengi. Amesema “viongozi wa dini mnao watu wengi nyuma yenu ambao ni waumini na wanawasikiliza hivyo mnawajibu wa kusaidia juhudi zinazofanywa na serikali za kuboresha maisha ya wananchi wake”. 

Akiongelea zoezi linaloendelea la uboreshaji daftari la wapiga kura, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa zoezi la uboreshaji daftari la wapiga kura linaendelea katika mkoa wa Iringa. Amesema kuwa changamoto ni kuwa mashine zinatumia umeme hivyo zinahitaji kuchajiwa na sehemu za vijijini hazina umeme. Amesema kuwa mkoa unakabiliana na changamoto hiyo ili kuhakikisha zoezi zima linakuwa na mafanikio. Amesema changamoto ya matumizi ya kopyuta limechukuliwa kwa uzito unaostahili na watu wenye uelewa wa kompyuta wamechukuliwa katika kufanya zoezi la uboreshaji daftari hilo ili liende vizuri na haraka.
 
Mkuu wa Mkoa Iringa na viongozi wa dini
Wakati huohuo, bibi. Masenza amewataka viongozi wa dini kuendelea kuwahamasisha waumini na wananchi kwa ujumla kuipitia na kuifahamu Katiba inayopendekezwa ili mwisho waweze kufanya maamuzi sahihi wananchi wenyewe pasipo kushurutishwa. Amesema kuwa Katiba hiyo imegusa maeneo na makundi yote ya kijamii hivyo ikisomwa kwa umakini itawasaidia wananchi ufanya maamuzi sahihi.

Katika kikao hicho mada juu ya hali ya lishe katika mkoa, hali ya maambukizi ya ukimwi na hali ya elimu ziliwasilishwa na kujadiliwa kwa kina. Viongozi hao wamekubaliana kukutana kila baada ya miezi nne na kujadili mambo muhimu katika mkoa wa Iringa.
=30=

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...