Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Shule za sekondari za Igowole na
Kawawa zimepongezwa kwa kufanya vizuri katika mitihani ya kidato cha sita mwaka
2014 na kuung’arisha mkoa wa Iringa kitaifa.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa
Kamati ya mitihani wa Mkoa wa Iringa, bibi. Wamoja Ayubu alipokuwa akiongea na
waandishi wa habari kuhusu mitihani inayoendelea ya kidato cha sita nchini
ofisini kwake.
Wamoja amesema “nichukue nafasi hii
kipekee kuzipongeza shule za sekondari za Igowole na Kawawa zote zipo katika
halmashauri ya wilaya ya Mufindi kwa kufanya vizuri katika mitihani ya kidato
cha sita mwaka 2014, ambapo Igowole iliahika nafasi ya kwanza kitaifa na Kawawa
ilishika nafasi ya kumi. Hongereni sana kwa matokeo hayo yaliyoufanya mkoa wetu
kung’ara.” “Aidha, nichukue nafasi hii pia kuzipongeza shule zote za mkoa wa
Iringa kwa kuwa kwa ujumla wake zilifanya vizuri katika matokeo hayo kati ya
shule 22 zilizokuwa na watahiniwa wa kidato cha sita mwaka 2014 shule 18
zilifaulisha kwa asilimia 100 kwa maana hakukuwa na mwanafunzi aliyepata daraja
la 0”, aliongeza bibi. Wamoja.
Akiongelea mitihani inayoendelea ya
kidato cha sita, Mwenyekiti wa Kamati ya Mitihani wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa
mkoa unavyo vituo 23 vya mtihani wa kidato cha sita vyenye jumla watahiniwa
2,162. Amesema kuwa vituo hivyo vitasimamiwa na wasimamizi 73 kati yao
wasimamizi wakuu 23 na wasimamizi wasaidizi kutoka nje wapatao 50.
Kwa mitihani ya ualimu, amesema vipo
vituo 4 vyenye jumla ya watahiniwa 324 kati yao 122 ni ngazi ya Cheti na 202
ngazi ya Diploma. Ameongeza kuwa vituo hivyo vitasimamiwa na wasimamizi wakuu
wanne na wasimamizi wasaidizi saba kutoka nje.
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Katibu
Tawala Mkoa wa Iringa amewataka wasimamizi kutokuwa na tamaa ya fedha
itakayowasababishia kujiingiza katika vitendo vya uvujishaji mitihani. Aidha,
amewataka kuzingatia ratiba zilizotolewa ili kila mtihani ufanyike kwa wakati
uliopangwa na kuwepo katika chumba cha mtihani kipindi chote ili kutotoa mwanya
kwa watahiniwa kutazamiana.
Wakati huohuo Mkuu wa Mkoa wa Iringa,
bibi. Amina Masenza amewatakia heri watahiniwa wote wa mitihani ya kidato cha
sita mkoani Iringa na kuwataka kutokuwa na hofu na kufanya mitihani hiyo kwa
kujiamini kwa kuzingatia yale yote waliyojifunza.
Mitihani wa kumaliza kidato cha sita
na ualimu imeanza tarehe 04 Mei na itaendelea hadi tarehe 27 nchini kote.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni