Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mamlaka
ya majisafi na usafi wa mazingira Iringa (IRUWASA) wametakiwa kutoa huduma bora,
kwa wakati na bei halali ili kuondoa malalamiko ya wateja.
Kauli
hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua taftishi
juu ya maombi ya kurekebisha bei za huduma ya majisafi na majitaka yaliyotolewa
na IRUWASA katika ukumbi wa Veta mjini Iringa.
Masenza alisema kuwa watumiaji wa huduma ya maji wanayo
haki ya kupata huduma kwa wakati, kwa bei halali, kuhoji ubora wa huduma wanayopata
na kutoa malalamiko kwa watoa huduma, na ikibidi kwa EWURA ili kero zote
ziondolewe. Alisema pamoja na haki hiyo, watumiaji wa huduma wanao wajibu, kwa
sababu “haki bila wajibu ni vurugu, na
wajibu bila haki ni utumwa”.
Alisema “watumiaji wa huduma za maji na uondoshaji wa
majitaka wana wajibu wa kulipia huduma hizo kikamilifu na kwa wakati muafaka.
Aidha, wanao wajibu wa kuithamini na kuihifadhi miundombinu iliyopo kwa manufaa
yao, watoa huduma na Taifa kwa ujumla”.
Kwa
upande wa watoa huduma, mkuu wa mkoa alisema kuwa kwa mujibu wa sheria, watoa huduma wanaodhibitiwa na EWURA
kama IRUWASA, wana wajibu wa kutoa taarifa sahihi za utendaji wao kwa wateja
wao na kwa EWURA. Alisema jukumu lao la msingi ni kutoa huduma na bidhaa bora
na kwa wakati kwa watumiaji wengi zaidi. Aliongeza kuwa watoa huduma wana haki
zao za msingi ikiwa ni pamoja na kupata marejesho ya mitaji yao na faida ili
waweze kuwekeza zaidi katika miundombinu na mambo mengine ili huduma kama za
majisafi na uondoshaji wa majitaka ziweze kuwafikia watu wengi zaidi.
Akiongelea matarajio ya serikali, alisema “serikali
inatarajia utendaji mahiri wa EWURA utakuwa chachu ya kuboresha utoaji wa
huduma za majisafi na uondoshaji wa majitaka hapa nchini. Uwekezaji katika
sekta hii utaongeza upatikanaji na ubora wa huduma hii na hivyo kuleta ufanisi
endelevu na wenye kuzingatia uboreshaji wa mazingira kwa faida yetu na ya
vizazi vijavyo” alisisitiza Masenza.
Alisema “taftishi hii ya leo ni miongoni
mwa juhudi za EWURA katika kushirikisha wadau na kupata maoni yao kuhusu huduma
zinazotolewa na IRUWASA na mipango itakayowasilishwa mbele yenu katika sekta
hii muhimu ya huduma za majisafi na uondoshaji wa majitaka. Sisi ndio watumiaji
wa huduma hizo na sisi ndio wenye maoni kuhusiana na ubora wa huduma
tunazozipata na changamoto mbalimbali zinazoendana na upatikanaji wa huduma
hizo”.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni