Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Watumishi
wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa wametakiwa kutoa taarifa zinazohusu
ukiukwaji wa maadili na uadilifu ili haki iweze kutendeka.
Kauli
hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa Kamati ya kudhibiti uadilifu katika ofisi ya
mkuu wa mkoa wa Iringa, Kilasi Mwakilasi alipokuwa akifafanua uwepo na utendaji
kazi wa kamati yake.
Mwakilasi
ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Miundombinu alisema kuwa kamati
ya kudhibiti uadilifu ni chombo kilichoundwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa
na serikali kwa ajili ya kuangalia maandili kikiwa na lengo la kusimamia na
kudhibiti utendaji wa kimaadili kwa watumishi wa nyanja zote katika ofisi ya
mkuu wa mkoa wa Iringa.
Alisema kuwa kamati hiyo inaangalia kwa kiasi gani
maadili yanafuatwa katika kuwahudumia wananchi na baina ya watumishi wenyewe. Alisema
kuwa chombo hicho bado hakifahamiki kwa watumishi wote pamoja na kuwa na jukumu
muhimu la kudhibiti katika utumishi ofisini hapo.
Mwalikasi
alisema kuwa katika ofisi ya mkuu wa mkoa, kamati hiyo inaangalia kuanzia kwa
viongozi waandamizi kama wakuu wa sehemu na vitengo wanatenda kazi kwa kufuata
maadili pasipo kuwanyanyasa wala kuwaonea watumishi walio chini yao. Pamoja na
mambo mengine masuala ya rushwa yanaangaliwa kwa uzito mkubwa. Aliyataja mambo
mengine kuwa ni unyanyasaji wa aina zote, uadilifu katika utoaji wa huduma kwa
wateja wa nje, matumizi ya lugha yenye staha na mavazi.
Akiongelea
hali ya maadili na uadilifu katika ofisi ya mkuu wa mkoa, Mwenyekiti wa kamati
ya kusimamia maadili alisema kuwa hali
ya maadili na uadilifu ni ya kuridhisha. Alisema kuwa kamati yake inajiridhisha
kutokana na kutokuwapo kwa malalamiko kutoka kwa watumishi na wapokea huduma wa
nje. Kwa upande wa changamoto, alisema kuwa kamati yake inakabiliwa na changamoto
ya kufahamika kwa watumishi pamoja na rasilimali bajeti. Aidha, aliwataka
watumishi wote pindi wanapokuwa na tatizo la kimaadili na uadilifu
kuliwasilisha katika kamati yake ili haki iweze kuchukua mkondo wake.
Kamati
ya kudhibiti maadili iliundwa na wajumbe wanne
kutoka sehemu ya miundombinu, utawala, elimu na afya waliochaguliwa kutokana na
kuwa na maadili mema katika jamii.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni