Watumishi
wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa wamepongezwa kwa utendaji kazi pamoja na changamoto
ya ufinyu wa bajeti.
Pongezi
hizo zilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa
akiongea na watumishi wote wa ofisi ya mkuu wa mkoa hivi karibuni katika ukumbi
wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa.
Wamoja
alisema “nianze kwa kuwapongeza watumishi wote kwa nafasi zenu kwa utendaji
kazi katika ofisi hii. Mafanikio ya mkoa yanatokana na utendaji wenu mzuri wa
kazi. Ni matumaini yangu mtaongeza juhudi zaidi katika mwaka huu wa fedha
2015/2016 pamoja na changamoto ya bajeti na rasilimali tuliyonayo”.
Amewataka
watumishi wote kufanya kazi kwa kujaliana na kusisitiza kuwa kidogo
kitakachopatikana kigawanywe kwa usawa na haki ili wote waweze kuwahudumia
wananchi vizuri. Amesema kuwa kwa kuwa muda mwingi watumishi wanautumia katika
maeneo yao ya kazi, wao ni familia moja hivyo suala la upendo ni muhimu sana. “Muda mwingi tunatumia ofisini
hivyo sisi ni ndugu. Mtu akiwa na shida hata kama huna uwezo wa kumtatulia hebu
mshauri. Lazima tuone namna gani tutapunguziana msongo wa mawazo” alisisitiza
Wamoja.
Akiongelea
kufanya kazi kwa uwazi, Katibu Tawala Mkoa wa Iringa aliwataka wakuu wa sehemu
na vitengo katika ofisi ya mkuu wa mkoa kufanya kazi kwa uwazi na
kuwashirikisha watumishi walio chini yao. Amesema “ushirikishaji ni jambo zuri
katika kuondoa manung’uniko ya watumishi. Cha msingi ni kupeana taarifa katika
sehemu na vitengo vyenu ili kuondokana na taarifa za upotoshaji zinazoweza
kujitokeza”.
Wakati
huohuo Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Utawala na Rasilimali watu Scolastica
Mlawi alitumia kikao hicho kuwakumbusha watumishi kuzingatia sheria na kanuni
za utumishi wa umma katika kipindi chote cha utumishi wao. Aidha, aliwakumbusha
watumishi kuwa wanawajibu wa kuwahi kazini na kutekeleza majukumu yao kwa
mujibu wa muundo wa utumishi. Alisema kuwa kila mtumishi anawajibu wa kusaini
kitabu cha mahudhurio kwa mujibu wa taratibu za ofisi.
Akiongelea mavazi, aliwataka
watumishi kuvaa vizuri kama waraka wa mavazi unavyoelekeza.
Kikao
baina ya Katibu Tawala Mkoa na watumishi ni muendelezo wa vikao vya kujadili
changamoto na mafanikio katika ofisi ya mkuu wa mkoa na kufahamishana hali
halisi ya ofisi inavyokwenda kwa kipindi husika.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni