Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa - IRINGA
Serikari mkoani Iringa imemaliza
mgogoro baina ya muwekezaja na wachimbaji wadogo katika machimbo ya dhahabu
katika kijiji cha Ulata.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa
habari ofisini kwake, mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza amesema kuwa mgogoro
huo ulikuwa baina ya muwekezaji katika machimbo hayo ya dhahabu Ibrahim Msigwa,
wachimbaji wadogo na kijiji cha Ulata.
Mkuu wa mkoa wa Iringa ambaye pia ni
mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa alilazimika kutembelea eneo la
mgogoro akiambatana na kamati yake ya ulinzi na usalama kuona hali halisi ya
eneo husika kufuatia vifo vya wachimbaji watano waliofukiwa katika moja ya
miduara katika machimbo hayo hivi karibuni.
Masenza aliyataja makubaliano yaliyofikiwa
baina ya muwekezaji, uongozi wa kijiji, wachimbaji wadogo na kamati ya ulinzi
na usalama mkoa kuwa ni muwekezaji katika machimbo hayo Ibrahim Msigwa mwenye
leseni sita za uchimbaji atoe hisa mbili kwa kila leseni na kukipatia kijiji
cha Ulata. Hisa hizo zilielekezwa kuwa zitatumika katika shughuli za maendeleo
za kijiji hicho. Makubaliano mengine yaliyofikiwa ni mwenyekiti wa kijiji cha
Ulata alitakiwa kuvaa vazi la uongozi na kuwaongoza wanakijiji kwa mujibu wa
taratibu na miiko ya uongozi ili kuhakikisha usalama unakuwepo katika kijiji
hicho. Pia ofisi ya madini kanda ya kusini magharibi ikakague usalama wa eneo
lote la machimbo.
Aidha, mwenyekiti alitakiwa kuitisha kikao cha kijiji na
kufafanua makubaliano hayo ili kijiji kiingie katika umiliki wa machimbo hayo
kihalali.
Wakati huohuo, mwenyekiti wa kamati
ya ulinzi na usalama mkoa wa Iringa aliitaka ofisi ya kanda ya madini
kuwajengea uwezo wachimbaji vijana ili wakopesheke waweze kuchimba kwa mujibu
wa taratibu na ufanisi. Aidha, amewataka wachimbaji vijana kuachana na tabia ya
anasa ikiwa ni pamoja na matumizi yaliyokithiri ya vilevi na kujilinda na
maambukizi ya virusi vya ukimwi katika eneo la machimbo. “Viroba vinawaua
wanangu na kuharibu mapafu. Mkishalewa hamuwezi kufanya maamuzi sahihi ikiwa ni
pamoja na kukumbuka kuwa kuna Ukimwi” alisisitiza Masenza.
Aliwakumbusha wachimbaji hao kuwa
hakuna mtu au kikundi cha watu kilicho juu ya sheria na kuwataka kufuata sheria na taratibu za
nchi. Amekemea tabia za kuwapiga na kuwafanyia vurugu maafisa wa serikali na
raia wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao. “Nchi hii ni huru na ni yetu sote,
hakuna aliye juu ya sheria na haki ya kupiga wengine na kuwafanyia vurugu.
Tabia hiyo ni marufuku katika mkoa ninaouongoza mimi” alisisitiza Masenza.
Nae Mhandisi Migodi, kanda ya kusini magharibi
Zephania Msungi alisema awali hali ilikuwa tete katika machimbo hayo kwa sababu
maafisa kutoka ofisi ya madini ya kanda hawakuruhusiwa kuingia katika eneo
hilo. Alisema kwa muafaka huo itakuwa rahisi kutekeleza jukumu lao la kusimamia
sheria ya madini ya mwaka 2010 na kanuni zake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha
serikali inapata mapato yake kutokana na shughuli za machimbo.
Akiongelea hali ya usalama katika
machimbo hayo ya dhahabu, Mhandisi Mgungi alisema kuwa hali ya usalama siyo ya
kuridhisha kwa sasa. Ofisi yake itaenda kukagua eneo hilo na kushauri juu ya
uchimbaji salama kwa usalama wa wachimbaji wenyewe.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni