Jumatano, 23 Septemba 2015

MKOA WA IRINGA WAFANIKIWA KUZUIA MIMBA ZA WANAFUNZI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkoa wa Iringa umejitahidi kudhibiti mimba kwa wasichana wa shule za msingi na kuongeza idadi ya wasichana wanaomaliza elimu ya msingi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa kamati ya mitihani mkoa wa Iringa, Mwl Euzebio Mtavangu alipokuwa akifafanua maandalizi ya mkoa wa Iringa katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2015 utakaofanyika kuanzia kesho nchini nzima.
Mwl Mtavangu ambaye pia ni Kaimu afisa elimu wa mkoa wa Iringa alisema kuwa mwaka 2015 idadi ya wasichana wanaomaliza elimu ya msingi ni kubwa ikilinganishwa na idadi ya wavulana kutokana na mkoa kudhibiti tatizo la mimba kwa wanafunzi wa kike katika shule za msingi. Alisema kuwa kati ya watahiniwa 21,323 wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2015, wasichana ni 11,448 na wavulana ni 9,875. Alisema kuwa tofauti na miaka ya nyuma ambayo idadi ya wasichana waliokuwa wakihitimu elimu ya msingi ilikuwa ndogo kutokana na wasichana wengi kupata ujauzito na kushindwa kumaliza elimu ya msingi. Alisema kwa kutambua umuhimu na nafasi ya mtoto wa kike katika jamii, mkoa wa Iringa utaendelea kudhibiti mimba kwa wasichana ili wote waweze kumaliza elimu ya msingi na kuchangia katika kukuza uchumi wa taifa. Akifafanua ongezeko hilo kwa kila halmashauri, alilitaja ongezeko hilo kwa kila halmashauri kama ifuatavyo; Manispaa ya Iringa Wasichana (1,748) na wavulana (1,534), halmashauri ya wilaya ya Iringa Wasichana (3,046) na wavulana (2,618), halmashauri ya wilaya ya Kilolo wasichana (3,088) na wavulana (2,776) na halmashauri ya wilaya ya Mufindi wasichana (3,566) na wavulana (2,947).
Mwl Mtavangu alisema kuwa jumla ya shule 457 zitafanya mhihani huo kwa mkoa wa Iringa, ikiwa ni Manispaa ya Iringa shule (41), halmashauri ya wilaya ya Iringa (142), halmashauri ya wilaya ya Kilolo (106) na halmashauri ya wilaya ya Mufindi (168). Alisema kuwa katika mtihani huo, jumla ya mikondo 977 katika shule hizo 457 itahusika ikiwa na wasimamizi 977.
Aliwataja watahiniwa wengine kuwa ni watahiniwa wasioona watano wasichana wakiwa watatu na wavulana wawili. Wengine ni watahiniwa wenye uono hafifu 33, wasichana (18) na wavulana (15).
Kwa upande wa shule zenye mchepuo wa kiingereza alisema kuwa shule hizo zipo 10 zenye jumla ya watahiniwa 455, wasichana wakiwa 222 na wavulana 233. Katika siku ya kwanza mitahani ya sayansi, hisabati na Kiswahili itafanyika ikifuatiwa na mitihani ya kiingereza na maarifa ya jamii.
Akiongelea matarajio ya ufaulu kwa mkoa wa Iringa, alisema kuwa mkoa unatarajia kupanda hadi nafasi ya pili kitaifa kutoka nafasi ya nne ya mwaka 2014 huku watahiniwa wakitarajiwa kufaulu kwa zaidi ya asilimia 75 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2014 wa asilimia 68.58. Ikumbukwe kuwa mkoa wa Iringa umekuwa ukishika kati ya nafasi ya tatu na nne kwa ufaulu wa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa miaka 18 mfululizo.
=30=

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...