Jumatano, 23 Septemba 2015

WANAWAKE IRINGA WATAKIWA KUPIMA SARATANI YA KIZAZI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wanawake mkoani Iringa wametakiwa kujitokeza kupima saratani ya mlango wa kizazi ili wanapogundulika na saratani hiyo waanze matibabu mapema.
Wito huo umetolewa na mganga mkuu wa mkoa wa Iringa, Dkt. Robert Salim alipokuwa akifungua semina ya kufuatilia utekelezaji wa mipango na maazimio yaliyowekwa kuhusu kukabiliana na saratani ya mlango wa kizazi iliyofanyika katika ukumbi wa chuo cha afya ya msingi mjini Iringa.
Dkt. Salim alisema kuwa saratani ya mlango wa kizazi inasababisha maradhi na vifo kwa wanawake wengi nchini isipotambuliwa na kuanza kutibiwa mapema. Alisema kuwa wanawake wote walioanza mahusiano ya kimapenzi wanatakiwa kujitokeza katika vituo vya afya kupima ili wanapogundulika wameathirika na saratani hiyo waanze tiba mapema. Alisema kuwa yapo mahusiano makubwa baina ya maambukizi ya virusi vya ukimwi na saratani ya mlango wa kizazi. Kutokana na mahusiano hayo ambayo kwayo mkoa wa Iringa umeathirika sana na maambukizi ya ukimwi kwa 9.1% hivyo kusababisha ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi kuwa juu.
Nae Mkurugenzi wa uboreshaji afya kutoka taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Dkt. Sarah Maongezi alisema kuwa semina hiyo ililenga kufuatilia utekelezaji wa mipango na maazimio ya awali waliyojiwekea katika kukabiliana na tatizo la saratani ya mlango wa kizazi mkoani hapa. Alisema kwa kuwa mkoa wa Iringa ulianza muda mrefu mapambano dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi hivyo mkoa unatakiwa kuwa umepiga hatua za mafanikio zaidi ikilinganishwa na maeneo mengine nchini. Alisema kuwa kwa hatua iliyofikiwa na mkoa wa Iringa, mkoa huo unaweza kujihamasisha kununua vifaa na vifaa tiba kwa lengo la kukabiliana na saratani ya mlango wa kizazi.
Saratani ya mlango wa kizazi ni miongoni mwa magonjwa yanayosababisha vifo kwa wanawake wengi ikikadiriwa kuwa zaidi ya wanawake 4,000 hupoteza maisha nchini kila mwaka.
=30=

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...