Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Halmashauri
ya Wilaya ya Kilolo imepanda miti zaidi ya milioni 15 katika jitihada za
utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwa mwaka 2015/2016.
Kauli
hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Rukia
Muwango alipokuwa akiwasilisha taarifa ya Wilaya hiyo katika kilele cha siku ya
Mazingira duniani iliyofanyika kimkoa Wilayani Kilolo.
Muwango
alisema kuwa Halmashauri yake inalipa kipaumbele suala ya utunzaji na uhifadhi
wa mazingira. “Kwa kipindi cha mwaka
2015/2016 Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo imepanda jumla ya miti 15,105,394 katika
maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya ya Kilolo na vikundi 16 vya wapandaji miti
vimeanzishwa katika maeneo mbalimbali. Aidha, tumeweza kutambua na kuvitunza
vyanzo vya maji 2,165” alisisitiza Muwango.
Aliongeza kuwa juhudi
zinaendelea kufanyika kuhakikisha kunakuwa na utunzaji endelevu wa mazingira
wilayani Kilolo. Alizitaja juhudi hizo kuwa ni kuzuia kilimo kufanyika katika
vyanzo vya maji, kuhamasisha upandaji miti na kuanzisha vikundi vya wapanda
miti. Juhudi nyingine ni kuhamasisha ufugaji nyuki pamoja na uandaaji wa
mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji ambapo maeneo ya matumizi mbalimbali
yametambuliwa. Alisema kuwa jumla ya vijiji 34 vimeandaliwa mpango wa matumizi bora
ya ardhi ya vijiji kwa kushirikiana na wadau.
Mkurugenzi
Mtendaji alizitaja changamoto za utunzaji wa mazingira kuwa ni mabadiliko ya
tabia nchi yanayopelekea kupotea kwa baadhi ya viumbe hai na milipuko ya
magonjwa. Changamoto nyingine ni ukataji miti ovyo ya asili na uchomaji moto
ovyo wa mapori na mbuga kwa baadhi ya maeneo.
Katika
kukabiliana na changamoto hizo, Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo inaendelea
kutoa elimu juu ya uhifadhi wa mazingira kwa kushirikiana na wadau na jumla ya
vijiji 45 zimepata elimu. Kutenga na kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri
katika kutekeleza shughuli za mazingira. Mkakati mwingine ni kusimamia sheria,
kanuni na taratibu zinazohusiana na utunzaji na uzuiaji wa uharibifu wa
mazingira na vyanzo vya maji.
Ikumbukwe
kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo ina jumla ya eneo la misitu la Hekta
255,039 kati yake Hekta 47,747 zinasimamiwa na vijiji, Hekta 9,968 zinasimamiwa
na Halmashauri ya wilaya na Hekta 197,592 zinasimamiwa na serikali kuu.
Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo imewekeza katika upandaji miti eneo lenye
ukubwa wa Hekta 190.545.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni