Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Sektretarieti
za mikoa zimetakiwa kusimamia uboreshaji wa miundombinu ya umwagiliaji maji ili
kudhibiti upotevu wa maji na kuyafikisha kwa wananchi wengi zaidi.
Kauli
hiyo ilitolewa na Mhandisi wa Maji Mkoa wa Iringa, Shaban Jellan alipokuwa
akifafanua majukumu ya Sekretarieti za Mikoa katika usimamizi wa rasilimali
maji katika kikao cha kujadili uhifadhi endelevu wa mto Ruaha Mkuu kilichofanyika
katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa.
Mhandisi
Jellan alisema kuwa katika kuhakikisha uhifadhi wa rasilimali maji, Sekretarieti
za mikoa zinawajibu wa kusimamia uboreshaji miundombinu ya umwagiliaji ili
kuhakikisha kuwa maji hayapotei ovyo na kuendelea kuwanufaisha wananchi wengi zaidi.
Alisema kuwa maji mengi yamekuwa yakipotea katika umwagiliaji kutokana na
miundombinu hiyo kuacha mianya ya upotevu wa maji hayo.
“Sekretarieti za mikoa zinawajibu wa
kusimamia, kufuatilia na kutoa ushauri juu ya utekelezaji wa majukumu ya
mamlaka za serikali za mitaa na taasisi zinazofanya kazi kwenye halmashauri”
alisisitiza Mhandisi Jellan. Aidha, aliongeza kuwa sekretarieti za mikoa
zinawajibu wa kuzisaidia mamlaka za serikali za mitaa katika kuandaa miongozo
kwa ajili ya utekelezaji na kuziwezesha na kuzishauri mamlaka hizo katika
uanzishaji, usajiri na uendeshaji wa jumuiya za watumia maji na kuzijengea
uwezo mamlaka za serikali za mitaa.
Alishauri
kuwa elimu iendelee kutolewa kwa jamii juu ya umuhimu wa utunzaji na matumizi
endelevu ya rasilimali maji. “Elimu
itaisaidia jamii katika utunzaji na uhifadhi wa vyanzo vya maji na kufanya
rasilimali hiyo kuwa endelevu” alisisitiza Mhandisi Jellan. Aliongeza kuwa
elimu hiyo iende sambamba na umuhimu wa kuandaa mipango ya matumizi bora ya
ardhi katika vijiji.
Vilevile,
alishauri kusimamia sheria na taratibu zilizopo na kuzifanyia marekebesho pale
inapobidi ili rasilimali maji iwe endelevu. Alisema kuwa baadhi ya wananchi na
mamlaka nyingine wamekuwa wakivunja sheria kwa maslahi yao binafsi na
kusababisha uhifadhi wa rasilimali maji kutokuwa wenye manufaa.
Akiongelea
mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya maji, Mhandisi wa maji mkoa wa Iringa
alisema kuwa mikoa kwa kushirikiana na ofisi ya bonde la mto Rufuji na mamlaka
za serikali za mitaa zilizopo kwenye bonde la mto Rufiji zimeanzisha jumuiya za
watumia maji 28. Halmashauri zimekuwa zikivitambua na kuvihifadhi vyanzo vya
maji katika maeneo yao kwa mujibu wa sera na sheria zilizopo. Mafanikio mengine
ni kutoa elimu juu ya sera na sheria za maji Na. 11 na 12 za mwaka 2009 na
sheria zingine zinazohusiana na mazingira.
Sekta
mahususi juu ya usimamizi wa rasilimali maji ni sekta za maji, kilimo,
maliasili na mazingira, ardhi na mifugo. Sekta hizo zinasimamia rasilimali maji
kwa mujibu wa sheria ya maji Na. 11 na 12 za mwaka 2009, sheria ya mazingira
Na. 20 ya mwaka 2004.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni