Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mamlaka
za Serikali za Mitaa mkoani Iringa zimetakiwa kuwajibika kwa wananchi kama
misingi ya demokrasia inavyoelekeza katika kutekeleza majukumu yao.
Kauli
hiyo ilitolewa na Afisa Uchunguzi wa Sektretarieti ya Maadili ya Viongozi wa
Umma, Elizabeth Komba alipokuwa akitoa mada juu ya Sheria ya Maadili ya
viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 na Kanuni za Maadili ya utendaji katika
utumishi wa Umma za mwaka 2003 kwenye semina ya viongozi wa Mamlaka za Serikali
za Mitaa iliyoandaliwa na Sektretarieti ya Maadili ya viongozi wa Umma na
kufanyika katika ukumbi wa Veta mjini Iringa.
Komba
alisema kuwa moja ya misingi ya demokrasia ni kuwa na serikali inayowajibika
kwa wananchi na yenye viongozi na watumishi wa umma wanaotumikia wananchi kwa
uadilifu. Alisema “serikali imepewa
dhamana tu ya kuajiri kwa niaba ya umma ndiyo maana hata mishahara ya watumishi
wa umma hulipwa kutokana na kodi za wananchi”. Alisema kuwa serikali huomba
kutumia fedha zitokanazo na kodi kwa kuwasilisha bajeti zao bungeni ambako
ndiko walipo wawakilishi wa wananchi.
Aliwakumbusha
viongozi hao kuwa uongozi ni dhamana waliyokabidhiwa na wananchi hivyo
wanatekeleza majukumu hayo kwa niaba ya wananchi. Aliongeza kuwa katika
kutekeleza dhama hiyo, viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa wanatakiwa
kutumia nyazifa zao kwa manufaa ya wananchi na siyo manufaa binafsi.
Komba
aliongeza kuwa ukosefu wa uadilifu, uwazi na uwajibikaji kwa baadhi ya viongozi
na watumishi wa umma katika kutekeleza majukumu ya umma huathiri utendaji kazi
na maamuzi katika ngazi mbalimbali.
“Dhana hii ya uadilifu, uwazi na uwajibikaji,
huitwa utawala bora, ikiwa na maana ya utawala wa sheria” alisisitiza
Komba. Aidha, aliongeza kuwa dhana ya utawala bora ni muhimu katika kutambua na
kuzingatia maadili yaliyowekwa na sheria katika shughuli za kali siku kwa
kusudi la kuleta maendeleo, kudumisha demokrasia kwa lengo la kuimarisha
serikali na jamii kwa ujumla.
Akiongelea
misingi na maadili ya uongozi wa umma kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sheria ya Maadili ya viongozi wa Umma ya
mwaka 1995 na Kanuni zake Ibara 135 (5) ya Katiba misingi ya maadili inapiga
marufuku mienendo na tabia inayofanya viongozi kuonekana hawana uaminifu na
uadilifu au kuonekana kukuza au kuchochea rushwa katika shughuli za umma.
Aliongeza
kutokana na maagizo ya katiba, sheria ya maadili ilitungwa ili kuweka na
kufafanua kwa kina misingi ya maadili ya viongozi. Maadili yaliyoainishwa
katika sehemu ya tatu ya sheria ni kujiepusha na migongano ya kimaslahi.
Maadili
mengine ni kutoa tamko la maslahi na tamko la rasilimali na madeni kila mwaka.
Pia kuepuka kupokea zawadi na fadhila za kiuchumi na kutotumia mali za umma kwa
maslahi binafsi. Maadili mengine ni kuepuka kuweka shinikizo lisilofaa katika
kuajiri, kupandisha vyeo ama kuchukua hatua za kinidhamu.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni