Ijumaa, 1 Julai 2016

IRINGA MANISPAA YAKOPESHA ZAIDI YA MIL 58 VIKUNDI VYA VIJANA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imekopesha zaidi ya shilingi milioni 58 vikundi 33 vya vijana kwa lengo la kuvijengea uwezo na mtaji ili viweze kutekeleza shughuli za uzalishaji mali.

Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Tawala katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Olgatho Mwinuka alipokuwa akisoma risala ya utii ya wananchi wa Manispaa ya Iringa kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2016 katika uwanja wa Mwembetogwa, Manispaa ya Iringa.

Mwinuka alisema kuwa katika kutekeleza kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka 2016 isemayo “vijana ni nguvu kazi ya taifa; washirikishwe na kuwezeshwa”, kwa mwaka 2016, Manispaa ya Iringa imekopesha shilingi
milioni 58,600,000 kwa vikundi 33 vya vijana vyenye jumla ya wanachama 419. Alisema kuwa lengo la mikopo hiyo ni kuwawezesha vijana kupata mitaji wa kuendesha shughuli zao za ujasiliamali. Aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2015/2016 Halmashauri hiyo ilitenga jumla ya shilingi milioni 212,956,061 kutoka mapato yake ya ndani kwa lengo la kuwawezesha vijana wajasiliamali kupata mikopo ya riba nafuu na kukuza mitaji yao.

Mwinuka alisema kuwa katika kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaaka huu, Manispaa ya Iringa inaendelea kukabiliana na changamoto za uhaba wa ajira kutokana na uwezo mdogo wa sekta binafsi kuzalisha ajira, ukosefu wa ujuzi na stadi za kazi, ukosefu wa taarifa sahihi za fursa na mitaji na maeneo ya kufanyia kazi kwa vijana.

Alisema kuwa katika kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo ili vijana washiriki katika maendeleo ya taifa, Manispaa ya Iringa imefanikiwa kuanzisha SACCOS ya vijana yenye wanachama 480 wakiwemo wanaume 268 na wanawake 212. SACCOS hiyo ilipatiwa mtaji wa shilingi 15,000,000 baada ya kujengewa uwezo wanachama na viongozi juu ya usimamizi na uendeshaji wake.

Akielezea maeneo yaliyotengwa kwa shughuli za vijana, “Halmashauri imetenga maeneo kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo katika kata za Kihesa ambapo kuna soko lililo katika hatua za ukamilishaji, kata ya kitwiru ambapo gulio limekamilika na wafanyabiashara wamepatiwa maeneo ya kujenga vibanda vya biashara na kata ya Ruaha ambapo ujenzi wa vibanda vya biashara kuzunguka soko unaendelea. Pia jumla ya maeneo 11 yametengwa katika michoro ya mipangomiji kwa ajili ya shughuli za vijana za kiuchumi, katika kata za Mwangata, Ruaha, Igumbilo, Kihesa, Isakalilo, Kitwiru, Mtwivila na Mkwawa” alisema Mwinuka.

Aidha, Halmashauri imeendelea kuhamasisha uundaji na usajili wa vikundi vya ujasiliamali na kiuchumi vya vijana, ambapo jumla ya vikundi 250 vyenye wanachama 6,250 wakiwemo wanawake 3,275 na wanaume 2,975 vimeundwa.
Mwenge wa Uhuru katika Manispaa ya Iringa ulikimbizwa umbali wa kilomita 64.4 katika kata saba, jumla ya miradi sita yenye thamani ya shilingi bilioni 7,139,993,299 imefikiwa, kati ya miradi hiyo mitatu ni ya huduma za kijamii, mmoja ni wa elimu, mmoja ni wa uzalishaji kupitia kilimo cha umwagiliaji na mwingine ni wa kuhifadhi na kutunza mazingira.
=30=

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...