Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Manispaa ya Iringa imefanikiwa kupima wanawake
wajawazito 6,853 waliohudhuria kliniki katika kutekeleza mkakati wa Mkoa wa
kupambana na Ukimwi wenye lengo la kupunguza kiwango cha maambukizi hadi
asilimia saba.
Taarifa hiyo
ilitolewa na Afisa Tawala katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Olgatho
Mwinuka alisema kuwa Manispaa ya Iringa katika kuendeleza mapambano dhidi ya Ukimwi
chini ya kaulimbiu isemayo “tanzania bila
maambukizi mapya, unyanyapaa na vifo vitokanavyo na ukimwi inawezekana” Manispaa
kwa kushirikiana na wadau inatekeleza mkaakti wa Mkoa wa kupambana na Ukimwi,
wenye lengo la kupunguza kiwango cha maambukizi toka asilimia 9.1 hadi asilimia
7 ifikapo mwaka 2017,
katika utoaji wa
huduma ya kuzuia maambukizi toka kwa mama kwenda kwa mtoto. Alisema kuwa jumla
ya wajawazito 6,853 walihudhuria kliniki ya afya ya uzazi kwa kipindi cha
Januari hadi Mei, 2016, kati yao 2,262 walipimwa maambukizi ya VVU, 122 sawa na
asilimia 5.4 walikutwa na maambukizi. Aidha, vituo vinavyotoa huduma hiyo
vimeongezeka toka 18 mwaka 2015 hadi 19 mwaka 2016.
Aliongeza kuwa Manispaa
kwa kushirikiana na wadau wake imeendelea kutoa elimu ya kujikinga na maradhi
ya Ukimwi kwa makundi yote. Kampeni ya tohara kwa wanaume inaendelea, ambapo
jumla ya wanaume 1,449 walitahiriwa kwa mwaka 2015. Vilevile, hamasa juu ya
upimaji na utoaji wa ushauri nasaha inaendelea kutolewa, ambapo watu 18,011
(8,167 me, 9,844 ke), kati yao 1,628 (634 me, 994 ke) sawa na 9% walikutwa na
maambukizi ya VVU kwa mwaka 2015.
Aidha, vituo vya
ushauri nasaha na upimaji vimeongezeka toka vituo 14 mwaka 2010 hadi vituo 18
mwaka 2016. Haki za watu wanaoishi na VVU/UKIMWI zimeendelea kutetewa kwa lengo
la kuondoa unyanyapaa na ubaguzi katika jamii.
Wakati
huohuo, afisa tawala huyo alisema kuwa mapambano
dhidi ya ugonjwa wa malaria, kupitia ujumbe usemao “wekeza katika maisha ya baadaye” chini ya kauli mbiu isemayo “tokomeza malaria” Manispaa inaendelea
kutoa elimu kuhusu namna malaria inavyoenezwa, jinsi ya kujikinga, upimaji wa
afya na matumizi ya dawa. Aliongeza kuwa elimu hiyo imepelekea kupungua kwa
ugonjwa wa malaria kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano, kutoka wagonjwa
30,795 mwaka 2012 hadi wagonjwa 4,620 mwaka 2015.
Vilevile, matumizi ya vyandarua yameendelea
kuhimizwa na katika kipindi cha mwezi Januari mpaka Machi 2016, jumla ya
vyandarua 113,418 vimegawiwa kwenye kaya 43,682 katika Manispaa ya Iringa.
Mwenge wa Uhuru katika Manispaa ya Iringa
ulikimbizwa umbali wa kilomita 64.4 katika kata saba, jumla ya miradi sita
yenye thamani ya shilingi bilioni 7,139,993,299
imefikiwa, kati ya miradi hiyo mitatu ni ya huduma za kijamii, mmoja ni wa
elimu, mmoja ni wa uzalishaji kupitia kilimo cha umwagiliaji na mwingine ni wa
kuhifadhi na kutunza mazingira.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni