Ijumaa, 1 Julai 2016

MBIJIMA ATAKA VIJANA KUELIMISHWA MADHARA YA RUSHWA



Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2016 George Mbijima ameitaka jamii kuwajengea uelewa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari juu ya madhara ya rushwa katika kupata haki na kujenga uchumi wa Taifa.

Mbijima alitoa kauli hiyo alipokuwa akitoa ujumbe wa Mwenge wa uhuru mwaka 2016 kwa wananchi wa mji wa Mafinga katika uwanja wa mashujaa mjini Mafinga.

Mbijima alisema kuwa mapambano dhidi ya rushwa si juhudi za Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) peke yake bali ni jukumu la jamii mzuma. “Umefika wakati wa kuwajengea uwezo na uelewa vijana wa shule za msingi na sekondari juu ya madhara ya rushwa kwa kupata haki ya mwananchi na madhara ya rushwa kwa uchumi wa Taifa” alisisitiza Mbijima. Aliongeza kuwa wapo watoto wa kike wanaonyanyasika katika mapambano yao ya kujiletea maendelea ya kielimu na kiuchumi kutokana na rushwa ya ngono na hatimae kupata Ukimwi. 

Alisisitiza kuwa vijana wajengewe utamaduni kwa kuchukia rushwa ili wawe wazalendo wa kweli kuwa kuichukia rushwa na mazingira yote yanayoashiria vitendo hivyo. Aliwataka vijana kuwa mstari wa mbele katika kufichua vitendo vya rushwa kwa kutoa taarifa Takukuru na kuwa tayari kutoa ushahidi pindi wanapotakiwa kufanya hivyo.

Akiongelea mapambano dhidi ya maambukizi ya ukimwi, kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa uhuru alisema kuwa lengo la Taifa ni kufikia sifuri tatu ifikapo mwaka 2030 nchini Tanzania. Alizitaja sifuri hizo tatu kuwa ni kuzuia maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi ili wasio na maambukizi wasipate na wenye maambukizi wasipate maambukizi mapya. Nyingine ni kuondoa unyanyapaa kwa kutokuwatenga wenye maambukizi kwa sababu hakuna aijuae kesho yake. 

Sifuri ya tatu aliitaja kuwa ni kuondoa vifo vitokanavyo na ugonjwa wa Ukimwi. “Katika kufanikisha mapambano hayo, wazizi waendelee kuwalea vijana katika maadili mema yanayozingatia maslahi ya nchi, vijana wakiachwa wenyewe wanapata fursa ya kujiingiza katika makundi maovu” alisisitiza Mbijima.
=30=


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...