Na Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa
Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo imepunguza
kiwango cha ugonjwa wa Malaria hadi kufikia asilimia 11.3 mwaka 2016.
Kauli hiyo hiyo ilitolewa na Katibu
Tawala Wilaya ya Kilolo, Yusuph Msawanga wakati akisoma risala ya utii ya
wananchi wa Wilaya ya Kilolo katika uwanja wa soko wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa
wilayani hapa.
Msawanga alisema kuwa ugonjwa wa Malaria
ni miongoni mwa magonjwa yanayoongoza kwa kuathiri watu wengi wilayani Kilolo.
“Kwa
kipindi cha mwaka 2016 kati ya wagonjwa 170,168 waliofika jengo la wagonjwa wa
nje 19,303 walipimwa na kugundulika kuwa na vimelea vya Malaria, hii ni sawa
asilimia 11.3 ya wagonjwa wote waliofika jengo la wagonjwa wa nje. Takwimu hizi
zinabainisha kuwa kiwango cha ugonjwa wa Malaria kilipungua kutoka asilimia
23.6 mwaka 2015 na kufikia asilimia 11.3 mwaka 2016” alisema Msawanga.
Aliongeza kuwa jumla ya wagonjwa
3,732 waliokuwa wamelazwa, kati yao 537 waligundulika kuwa na malaria baada ya
kupimwa sawa na asilimia 14.4 ya wagonjwa wote waliolazwa. Alisema kuwa kiwango
cha ugonjwa wa malaria kimepungua kwa asilimia 6.5 toka asilimia 20.9 ya mwaka
2014 hadi 14.4 mwaka 2016.
Katibu Tawala huyo katika kuhakikisha
ugonjwa wa Malaria unakuwa historia, wilaya ya Kilolo inaendelea kuielimisha
jamii juu ya matumizi ya sahihi ya vyandarua, kupima na kutoa tiba sahihi kwa
wagonjwa wa Malaria.
Juhudi nyingine alizitaja kuwa ni kuihamasisha
jamii kupima mapema mara wanapohisi kuumwa. Nyingine ni utoaji wa dawa za tiba
kinga kabla ya madhara kwa kutumia dawa ya mseto kwa mama wajawazito na
kuhamasisha jamii juu ya usafi wa mazingira ili kuondoa uwezekano wa mazalia ya
mbu waenezao Malaria.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni