Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Kamati
ya ulinzi na usalama mkoa wa Iringa imepongezwa kwa kusimamia amani na usalama
mkoani hapa.
Pongezi
hizo zilitolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa
alipokuwa akiongea na watumishi wa shamba la mifugo la Asas na wananchi wa Iringa
kwa ujumla alipofanya ziara fupi ya kukagua shamba hilo lililopo Igingilanyi
wilayani Iringa.
Majaliwa
alisema “leo napita kwenye shamba hili ila
ziarani nitapita kiwanadani. Muhimu zaidi ni ulinzi na usalama. Pongezi kwa
kamati ya ulinzi na usalama mkoa kusimamia amani na usalama. Endeleeni kuhakiki
uingiaji holela wa raia wa kigeni. Uhamiaji imarisheni ulinzi katika mipaka.
Tuendelee kuilinda nchi na mipaka yake”.
Akiongelea
matumizi ya ardhi, Waziri Mkuu alizitaka Halmashauri zote kusimamia matumizi bora
ya ardhi. Alizitaka Halmashauri kuhakikisha kila mwenye nyumba anapewa hati.
Aliziasa Halmashauari kuwa makini na utoaji wa hati mbili kwa kiwanja kimoja. “Halmashauri punguzeni migogoro hii. Wote
tunaowagawia mashamba makubwa wapewe hati za umiliki kwa miaka iliyowekwa kwa
mujibu wa sheria” alisisitiza Majaliwa.
Waziri
Mkuu alisema kuwa wengi wenye mifugo, hawaifugi bali wanaichunga. Alisema
mifugo ni mingi ila haijaleta tija kwa wenye mifugo. Alizitaka Sekretarieti za
mikoa kutoa elimu kwa wafugaji ili wafuge kisasa. Katika kuondoa migogoro baina
ya wafugaji na wakulima, Waziri Mkuu aliagiza mifugo yote nchini kuwekwa alama
ya utambulisho wa eneo husika.
Kuhusu
ufugaji katika shamba la mifugo la Asas, Majaliwa alisema “tunayo sababu ya kuendelea kumuunga mkono Asas kwa sababu anafuga
kitaalam, katika mashamba yake ameajili watu wengi. Asas pia ananunua bidhaa za
wafugaji wanaomzunguka. Endelea
kupanua shamba, na serikali itakuunga mkono. Wewe unaunga mkono moja kwa moja
azma ya serikali ya awamu ya tano na kuwa nchi ya viwanda”.
Waziri
Mkuu alifanya ziara fupi katika shamba la mifugo mkoani Iringa wakati akiwa
njiani kuelekea ziarani mkoani Njombe.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni