Na Mwandishi Maalum Iringa
Serikali
imesema kuwa watu wengi wamekuwa wakipoteza haki zao za msingi kutokana na
kutokujua kusoma na kuandika nchini.
Kauli
hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mafunzo ya
Ufundi, Mhandisi Stella Manyanya alipokuwa akiongea na wananchi wa kata ya
Ibumu wilayani Kilolo jana.
Mhandisi
Manyanya alisema “ndugu zangu, kutokujua
kusoma na kuandika kumewafanya wananchi wengi kupoteza haki zao katika kupiga
kura. Wapo watu wamedanganywa na kushindwa kufanya maamuzi sahihi wakati wa
upigaji kura. Watu wengine kwa kutokujua kusoma na kuandika wameibiwa katika
kufanya miamala ya fedha.
Aidha, siri za watu zimewekwa hadharani na watu ambao
waliwaamini. Hivyo, kujua kusoma na kuandika ni jambo la msingi sana”.
Aidha,
aliutaka uongozi wa wilaya ya Kilolo kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa
kwenda shule anapelekwa ili kuondoa tatizo la ucheleweshaji watoto kuanza
shule. Alisema kuwa kuwachelewesha watoto kuanza shule kunapelekea baadhi yao
kulazimika kuanza kujifunza elimu kupitia mfumo usio rasmi na Memkwa. Kupitia
mfumo usio rasmi baadhi yao wamekuwa wakiishia njiani kutokana na kukata tamaa.
“Katika hili la kupeleka mtoto shule,
mzazi au mlezi yeyote atakayekaidi achukuliwe hatua. Wazazi na walezi wameacha
kupeleka watoto wao shule, kutwa wanawapeleka mkoani Dar es Salaam kufanya kazi
za ndani. Kama ni kufanya kazi waende baada ya kumaliza shule. Watoto wadogo
hata maana ya kazi na mshahara hawajafahamu” alisisitiza Mhandisi Manyanya.
Naibu
Waziri alisema kuwa suala la kusoma na kuandika katika jamii ni la muhimu sana
na halitakiwi kuonewa aibu. “Tusilionee
aibu suala hili. Wabunge kama kweli tunawapenda wananchi wetu, lazima
tuwahimize kusoma na kuandika. Jambo hili litafanya tuache kumbukumbu na
historia nzuri kwenye majimbo yetu” alisisitiza Mhandisi Manyanya.
Katika
kuhakikisha jamii inajua kusoma na kuandika, aliagiza kuanzishwa kwa madarasa
ya watu wazima katika maeneo mbalimbali ili watu waliokosa fursa hiyo waweze
kuipata nje ya mfumo rasmi na elimu hiyo ipewe uzito mkubwa.
Ikumbukwe
kuwa mkoa wa Iringa una kiwango cha asilimia 18 cha watu wasiojua kusoma na
kuandika.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni