Jumamosi, 28 Januari 2017

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA UKOMA DUNIANI



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA UKOMA DUNIANI
Siku ya Ukoma Duniani huadhimishwa Duniani kote kila Jumapili ya mwisho wa mwezi Januari ya kila mwaka.

Mkoa wa Iringa kama maeneo mengine Duniani utaadhimisha siku hiyo kwa kutoa elimu kwa jamii juu ya ugonjwa wa ukoma, jinsi unavyoambukizwa, njia za kujikinga na ugonjwa huo, matibabu na madhara yatokanayo na ugonjwa huo.

Maadhimisho ya Siku ya Ukoma Duniani, mwaka 2017 yanaongozwa na Kaulimbiu isemayo “TUEPUKE ULEMAVU UNAOTOKANA NA UKOMA MIONGONI MWA WATOTO”.

Kauli mbiu hii imewalenga watoto mwaka kutokana na ukweli kwamba watoto kinga zao za mwili bado hazijaimarika vizuri hivo ni rahisi kupata maambukizi.
UKOMA ni miongoni mwa magonjwa ya zamani sana  husababisha  ulemavu wa kudumu mara mgonjwa anapochelewa kuanza huduma kote Duniani.
Pia imekua ni sababu kubwa  ya unyanyapaa katika jamii.

HALI YA UGONJWA WA UKOMA
KITAIFA
Ukoma unapungua  lakini bado mikoa 10 ambayo bado ina wagonjwa wengi kama LINDI,MTWARA,PWANI,MOROGORO,TANGA,GEITA,KIGOMA ,RUKWA,RUVUMA ,TABORA

Tumefikia viwango vya utokomezaji 2006,yaani chini ya mgonjwa 1 kati ya watu 10,000.Hapo mwaka 1983 walikua wanaripotiwa wagonjwa takriban 35000 ukilinganisha na mwaka  2011 waliripotiwa wagonjwa 1970 hii inaonyesha kupungua kwa ugonjwa huu baada ya kupatikana matibabusiku hadi siku.

Tatizo kubwa la ukoma ni kusababisha ulemavu wa kudumu,takribani walemavu wapya 250 kila mwaka  wanapatikana Tanzania kutokana na ukoma .
Mwaka 2015 walemavu walikua 300.

KIMKOA
Kwa mkoa wa iringa hali sio mbaya ugonjwa unapungua na tayari tumefikia viwango vya  utokomezaji   sasa tunaona wagonjwa wapya  10 mpaka 20 kwa mwaka.

Halmashauri ambazo zinaongoza na wagonjwa wengi wa ukoma ni Halmashauri ya wilaya ya Iringa na wilaya ya kilolo.

Hii inapelekea lengo la Shirika la Afya Duniani kuripoti chini ya mgonjwa mmoja kwenye jumla ya watu 10,000.

Huduma za matibabu na zile za kupunguza ulemavu hutolewa bila malipo

MAAMBUKIZI UKOMA
Ugonjwa wa Ukoma unaambukizwa kwa njia ya hewa kutoka kwa mtu mwenye maambukizi kwa kupiga chafya au kukohoa.

Ugonjwa wa Ukoma hauwezi kuambukizwa kwa kugusana ngozi na mgonjwa wa Ukoma.

UGONJWA WA UKOMA NI NINI?
Ni ugonjwa sugu wa kuambukiza unaosababishwa na Bacteria aitwae MYCOBACTERIUM LEPRAE. Bacteria wa aina hii hukaa muda mrefu mwilini kabla ya kuanza kuonekana dalili za ugonjwa. Bacteria hawa huathiri neva za mfumo wa fahamu hususani miguu, mikono na uso na ngozi. 

Ugonjwa wa ukoma unaathiri makundi yote katika jamii, haubagui taifa, rangi, umri wala jinsia ya mtu.

AINA ZA UGONJWA WA UKOMA;
Zipo aina 2 za ugonjwa wa Ukoma:
1.           Ukoma Mkali (Multibacillary). Aina hii ya Ukoma inatokana na vimelea vingi mwilini, ambapo mabaka yanakuwa zaidi ya matano mwilini.
2.           Ukoma wa kawaida (Paucibacillary). Aina hii ya Ukoma inatokana na vimelea vichache mwilini, ambapo mabaka yanakuwa chini ya mabaka matano mwilini.
Ugonjwa wa Ukoma una uhusiano mkubwa na kinga ya mwili wa binadamu. Mtu mwenye kinga ya mwili dhaifu nafasi ya kupata maambukizi na kuugua ugonjwa wa Ukoma ni kubwa zaidi ikilinganishwa na mtu mwenye kinga ya mwili imara.
Uhusiano baina ya ugonjwa wa Ukoma na umasikini ni mkubwa. Hii ni kutokana na ukweli kuwa umasikini unamfanya mtu kukosa uhakika wa mlo kamili jambo linalomsababishia kuwa ana lishe duni na kufanaya kinga yake ya mwili kuwa chini. Aidha, elimu na wigo wa kupata taarifa kwa mtu masikini ni mdogo sana. Mtu huyo hawezi kupata elimu na taarifa sahihi kuhusu ugonjwa wa Ukoma na njia sahihi za kujikinga na tiba iwapo ameambukizwa.

Kikawaida inachukua muda mrefu sana toka mtu kuambukizwa hadi dalili za ugonjwa wa Ukoma kuanza kuonekana. Muda huo unaweza kuwa kuanzia miaka 3 hadi miaka 30. Muda huo unategemea na kinga ya mwili ya mtu aliyeambukizwa. Kama kinga yake ya mwili ni imara dalili zitachelewa sana kuonekana lakini kama kinga yake ya mwili ni dhaifu dalili za ugonjwa wa Ukoma zitaonekana mapema.

Dalili za wazi za ugonjwa wa Ukoma ni:-
·         Mabaka kwenye ngozi moja au zaidi  ambayo hayana hisia.
    Baka hua na rangi iliyofifia  zaidi kuliko rangi ya kawaida ya ngozi.
·         Ganzi hasa kwenye viganja, mikono na miguu; hii inasababishwa na ukweli kuwa ugonjwa wa Ukoma unaathiri mishipa ya fahamu.
·         Uvimbe usio na maumivu usoni au  kwenye masikio
·         Ngozi kua na hisia kama moto
·         Pia mgonjwa huweza kufika kituo cha huduma na majeraha ya vidonda vilivyosababishwa na moto.

MATIBABU
Ukoma unatibika. Kwa miaka mingi, ugonjwa wa Ukoma haukuwa ukitibika, hivyo, uliwasababushia wagonjwa wengi kutengwa. Leo hii ugonjwa wa Ukoma unatibika. Shirika la afya duniani lilianzisha matibabu ya ukoma Nchini mwaka 1983 kufikia mwaka 1990 nchi nzima dawa zilikua zinapatikana.

 Dawa zipo katika vituo vyote vya kutolea huduma mgonjwa anapotambulika waratibu husimamia zoezi hilo, na matibabu yake ni bure. Matibabu huchuhua mwaka 1-2, kuwa kutegemeana na aina ya Ukoma.

Dawa zinapatikana bila malipo yoyote,tayari serikali imeshagharamia kupitia wadau wa maendeleo.

WITO:
  • Jamii iendelee kuelimishwa juu ya kikohozi salama kwasababu kwa njia ya hewa mtu aweza kuambukizwa.
  • Jamii iendelee kuelimishwa juu ya kuwahi uchunguzi pindi mtu anapoona dalili za ugonjwa wa Ukoma kama baka au mabaka yanapojitokeza katika mwili wake.
  • Kuimarisha kinga za mwili kwa kupima afya mapema, kupata ushauri wa kitaalamu na lishe bora.
  • Kuishi kwenye nyumba bora zenye madirisha makubwa yanayoruhusu hewa kuzunguka.
  • Kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya dalili za ugonjwa wa Ukoma, matibabu yake na njia za kujikinga.
Imeandaliwa   na:
Dr. Tecla Orio,
Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma
IRINGA


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...