Jumanne, 25 Aprili 2017

IHEMI WATAKIWA KUFANYA ULINZI SHIRIKISHI VYANZO VYA MAJI



Na. Dennis Gondwe, Iringa
Serikali ya Kijiji cha Ihemi imetakiwa kufanya ulinzi shirikishi kulinda chanzo cha maji cha Ihemi ili kiendelee kutiririsha maji muda wote.

Agizo hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa kikosi kazi namba tatu cha kunusuru ikolojia ya bonde la mto Ruaha mkuu ili liweze kurudi katika hali yake ya kawaida ambaye pia ni Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu jana katika kijiji cha Ihemi kilichopo katika kata ya Ifunda wilayani Iringa.
Mwenyekiti wa Kikosi kazi namba 3 Wamoja Ayubu akitoa maelekezo

Ayubu alisema “serikali ya kijiji cha Ihemi inawajibu wa kulinda chanzo cha maji hiki cha Ihemi. Tena ulinzi huu lazima uwe shirikishi ukihusisha wanufaika wote, hasa wakulima na wafugaji”. Aliongeza kuwa mifugo imekuwa ikilishwa katika chanzo hicho cha maji na kupiga marufuku utaratibu huo wa kulisha mifugo katika chanzo hicho. 
Aidha, aliitaka Halmashauri ya wilaya ya Iringa kutoa ushauri wa kitaalamu katika kutatua changamoto za kiuhifadhi kwa vijiji vyote vinavyozunguka vyanzo vya maji wilayani humo. “Halmashauri ya wilaya ya Iringa nyie ndiyo wasimamizi wa hivi vijiji, pia mnao wataalamu wa kutosha, hivyo, hakikisheni mnavitembelea vyanzo hivyo vya maji na kushauri kitaalamu juu ya uhifadhi wake ili viwe endelevu” alisisitiza Ayubu.

Awali Diwani wa Kata ya Ifunda, Elikus Ngweta alikiomba kikosi kazi hicho kuangalia uwezekano wa kuijengea uwezo jumuiya ya watumia maji bonde dogo la mto Lyandembela ili iweze kutekeleza majukumu yake vizuri. Vilevile, aliahidi kuendelea kusimamia utunzaji wa vyanzo vya maji katika Kata ya ifunda. “Mheshimiwa mwenyekiti wa kikosi kazi hiki, tunaahidi kutokana na umuhimu wa maji na kuwa maji ni uhai, na bila maji hakuna maisha, sisi tutasimamia utunzaji wa vyanzo vya maji ili viwe endelevu” alisisitiza Ngweta.

Kikosi kazi cha kurudisha ikolojia ya bonde la mto Ruaha mkuu kiliundwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
=30=

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...