Jumanne, 25 Aprili 2017

ASILIMIA 60 MAJI YANAPOTELEA KWENYE MIFEREJI ISIYOSAKAFIWA



Na Dennis Gondwe, Iringa
Wastani wa asilimia 60 ya maji yanapotea yanapopita katika mifereji ambayo haijasakafiwa na kuchangia katika upungufu wa maji kwenye mzunguko wake.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu baada ya kikosi kazi namba tatu kukagua mfereji wa asili katika skimu ya umwagiliaji ya Mkombozi inayohudumia vijiji sita katika kata za Mboliboli na Itunundu katika tarafa ya Pawaga wilayani Iringa jana alipoongoza kikosi kazi cha kunusuru ikolojia ya bonde la mto ruaha.

Ayubu alisema kuwa jitihada zinahitaki kuhifadhi mazingira yanayozunguka skimu ya umwagiliaji ya mkombozi yenye mfereji wa asili. Aidha, amepiga marufuku matumizi ya pampu za kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji kwa sababu hakuna kibali kilichotolewa kwa matumizi ya pampu katika skimu hiyo. “Matumizi ya pampu ni marufuku kuanzia leo. Pampu zote ziondolewe katika skimu hii kwa sababu zipo kinyume na sheria” alisisitiza Ayubu.

Ayubu aliongeza kuwa jamii nzima inategemeana katika uhitaji na matumizi ya maji na kusisitiza umakini katika matumizi yake. “Sote tunategemeana. Maji yakitoka hapa yanaenda kuzalisha umeme bwawa la mtera, yakitoka bwawa la mtera yanaenda kuzalisha umeme Kidatu, yakitoka kidatu yanaenda katika mashamba ya miwa kilombero” alisema Ayubu.

Wakati huohuo, mwenyekiti wa kikosi kazi hicho aliwataka wafugaji wenye mifugo mingi kujipanga kuvuna mifugo yao ili iendane na ukubwa wa ardhi iliyopo. Alisema kuwa wingi wa mifugo hauendani na tija inayotokana na mifugo hiyo zaidi ya kusababisha uharibifu wa mazingira.

Nae wakili wa serikali mkuu Benard Kongola kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) alisema kuwa mwananchi yeyote atakaye kamatwa akijihusisha na shughuli za kilimo ndani ya eneo la mita 60 kutoka ukingo wa mto ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria. Aidha, aliwataka wale wote wanaojishughulisha na kilimo ndani ya eneo hilo kuacha kabla ya zoezi la kuwakamata litakapoanza baada ya wiki moja.
=30=

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...