Jumanne, 25 Aprili 2017

SERIKALI YASHIRIKISHA ULINZI IKOLOJIA MTO RUAHA



Na. Dennis Gondwe, Iringa
Serikali imeamua kushirikisha jamii katika kurudisha hali ya ikolojia ya bonde la mto Ruaha mkuu ili liendelee kunufaisha watu na mifugo nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na mjumbe wa kikosi kazi cha kurudisha hali ya ikolojia katika bonde la mto Ruaha mkuu, Abbas Kandoro alipokuwa akielezea lengo la kikosi kazi kilichoundwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa wajumbe wa jumuiya ya watumia maji bonde dogo la mto Lyandembela katika mji mdogo wa Ifunda wilayani Iringa jana.

Kandoro alisema “serikali imeona ishirikishe wananchi ili hali ya ikolojia katika bonde la mto Ruaha mkuu irudi katika uhalisia wake. Ushirikishaji huu unalenga kuweza kupata maoni yenu ili kufahamu hatua za kufanya katika kurudisha hali ya mto Ruaha mkuu kwa kuwanufaisha wale wote wanaonufaika na mto huu”. 

Aliongeza kuwa eneo la bonde dogo la mto Lyandembela lina mchango mkubwa kwa upatikanaji wa maji yanayoingia katika mto Ruaha. “Hapa Ifunda tuna mto Lyandembela ambao maji yake yanazidi kupungua, hivyo kupunguza sana maji yanayoingia katika mto Ruaha. Mtakubaliana nami kuwa mambo yanayochangia ni uharibifu wa vyanzo vya maji hasa ukataji miti”. Sababu nyingine ni kulima katika vyanzo vya maji na matumizi ya pumpu za kumwagilia maji katika maeneo ambayo hayaruhusiwi kwa mujibu wa sheria.

Akiongelea mikakati ya kijiji ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira, katibu wa jumuiya ya watumia maji bonde dogo la mto Lyandembela (Jubodomlya), Elikus Ngweta aliitaja kuwa ni kuhakikisha watu wote wanaolima ndani ya mita 60 kuondoka ili kupisha uhifadhi endelevu wa bonde hilo. Mikakati mingine aliitaja kuwa ni kuielimisha jamii juu ya kutambua athari zinazotokana na uharibifu wa vyanzo vya maji na kupeleka elimu katika shule za msingi. Aliongelea pia kupanda miti ratiki ya maji kwenye maeneo ya vyanzo vya maji na miti mingine nje ya vyanzo vya maji ili isaidie kuvuta mvua.
 
Katibu wa jumuiya ya watumia maji bonde dogo la mto Lyandembela Elikus Ngweta (kushoto) akimuonesha mwenyekiti wa kikosi kazi hali ya mazingira

Mkakati mwingine ni kusimamia sheria kwa sababu jumuiya imesajiliwa kwa mujibu wa sheria. “Tunasimamia sheria ndogo baada ya kupitishwa na vikao halali na baadhi ya watu wamefikishwa mahakamani. Tukumbuke kuwa jumuiya ina vijiji 24 mpaka sasa” aliongeza Ngweta. Aliongeza kuwa kutokana na mikakati hiyo, vyanzo vinne vya maji ambavyo vilikuwa vimekauka vimeanza kutiririsha maji tena jambo linaloonesha hali ya matumaini mema.

Wakati huohuo, mwenyekiti wa kijiji cha Ifunda, Kayosi Kihwele alisema kuwa vyanzo 11 vya maji vimehifadhiwa na mikakati ya kuvilinda inaendelea kutekelezwa. “Katika utunzaji wa vyanzo vya maji, wapo baadhi ya wananchi wanaokaidi hasa kulima ndani ya mita 60 kutoka katika kingo za mito. Utaratibu wa kisheria umekuwa ukichukuliwa dhidi yao. Aidha, kijiji kimekuwa kikipanda miti rafiki ya maji kwa lengo la kufanya uendelevu wa mito iliyopo” alisema Kihwele.

Nae Bernard Mtove alisema pamoja na kazi nzuri zinazofanywa na timu za ufuatiliaji na taarifa nzuri kuandikwa ni vizuri utekelezaji ukatiliwa mkazo. “Kwa umri nilio nao uharibifu wa mazingira ni mkubwa kuliko elimu inayotolewa. Nikiwa mdogo tulikuwa tunachota maji karibu na nyumbani kadri siku zinavyoenda maji yanazidi kupungua” alisema Mtove.

Mwenyekiti wa kikosi kazi namba tatu ambaye pia ni Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipongeza juhudi za uhifadhi mazingira unaofanywa na kata ya Ifunda. Aidha, aliagiza uongozi wa kata ya Ifunda kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na kamati ya mazingira. “Kila kijiji lazima kiwe na kamati ya mazingira na kamati hizi ziundwe kwa kujibu wa sheria. Miongoni mwa majukumu ya kamati hizi ni kuangalia na kusimamia vyanzo vya maji katika maeneo husika. Katika uundwaji wa kamati hizi, uwiano wa kijinsia lazima uzingatiwe” alisisitiza Ayubu.

Kikosi kazi cha kurudisha hali ya ikolojia katika bonde la mto Ruaha kiliundwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan. Kikiwa katika kata ya Ifunda kiliongea na wajumbe wa jumuiya ya watumia maji bonde dogo la mto Lyandembela, kukagua chanzo cha maji cha Mkaa, chanzo cha maji cha Kivalali na chanzo cha maji cha Ihemi.
=30=

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Habari zinazoendelea hivi sasa

SERIKALI KUWEZESHA VIJANA KUKOPA

Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwatengenezea mazingira mazuri ya mikopo ili waweze k...