Na. Dennis Gondwe, Iringa
Serikali
imeamua kushirikisha jamii katika kurudisha hali ya ikolojia ya bonde la mto
Ruaha mkuu ili liendelee kunufaisha watu na mifugo nchini.
Kauli
hiyo ilitolewa na mjumbe wa kikosi kazi cha kurudisha hali ya ikolojia katika
bonde la mto Ruaha mkuu, Abbas Kandoro alipokuwa akielezea lengo la kikosi kazi
kilichoundwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu
Hassan kwa wajumbe wa jumuiya ya watumia maji bonde dogo la mto Lyandembela
katika mji mdogo wa Ifunda wilayani Iringa jana.
Kandoro
alisema “serikali imeona ishirikishe
wananchi ili hali ya ikolojia katika bonde la mto Ruaha mkuu irudi katika
uhalisia wake. Ushirikishaji huu unalenga kuweza kupata maoni yenu ili kufahamu
hatua za kufanya katika kurudisha hali ya mto Ruaha mkuu kwa kuwanufaisha wale
wote wanaonufaika na mto huu”. Aliongeza kuwa eneo la bonde dogo la mto
Lyandembela lina mchango mkubwa kwa upatikanaji wa maji yanayoingia katika mto
Ruaha.
“Hapa Ifunda tuna mto Lyandembela
ambao maji yake yanazidi kupungua, hivyo kupunguza sana maji yanayoingia katika
mto Ruaha. Mtakubaliana nami kuwa mambo yanayochangia ni uharibifu wa vyanzo
vya maji hasa ukataji miti”. Sababu nyingine ni kulima katika vyanzo vya
maji na matumizi ya pumpu za kumwagilia maji katika maeneo ambayo hayaruhusiwi
kwa mujibu wa sheria.
Akiongelea
mikakati ya kijiji ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira, katibu wa jumuiya
ya watumia maji bonde dogo la mto Lyandembela (Jubodomlya), Elikus Ngweta
aliitaja kuwa ni kuhakikisha watu wote wanaolima ndani ya mita 60 kuondoka ili
kupisha uhifadhi endelevu wa bonde hilo. Mikakati mingine aliitaja kuwa ni
kuielimisha jamii juu ya kutambua athari zinazotokana na uharibifu wa vyanzo
vya maji na kupeleka elimu katika shule za msingi. Aliongelea pia kupanda miti
ratiki ya maji kwenye maeneo ya vyanzo vya maji na miti mingine nje ya vyanzo
vya maji ili isaidie kuvuta mvua.
Mkakati
mwingine ni kusimamia sheria kwa sababu jumuiya imesajiliwa kwa mujibu wa
sheria. “Tunasimamia sheria ndogo baada
ya kupitishwa na vikao halali na baadhi ya watu wamefikishwa mahakamani.
Tukumbuke kuwa jumuiya ina vijiji 24 mpaka sasa” aliongeza Ngweta.
Aliongeza kuwa kutokana na mikakati hiyo, vyanzo vinne vya maji ambavyo
vilikuwa vimekauka vimeanza kutiririsha maji tena jambo linaloonesha hali ya
matumaini mema.
Wakati
huohuo, mwenyekiti wa kijiji cha Ifunda, Kayosi Kihwele alisema kuwa vyanzo 11
vya maji vimehifadhiwa na mikakati ya kuvilinda inaendelea kutekelezwa. “Katika utunzaji wa vyanzo vya maji, wapo
baadhi ya wananchi wanaokaidi hasa kulima ndani ya mita 60 kutoka katika kingo
za mito. Utaratibu wa kisheria umekuwa ukichukuliwa dhidi yao. Aidha, kijiji
kimekuwa kikipanda miti rafiki ya maji kwa lengo la kufanya uendelevu wa mito
iliyopo” alisema Kihwele.
Nae
Bernard Mtove alisema pamoja na kazi nzuri zinazofanywa na timu za ufuatiliaji
na taarifa nzuri kuandikwa ni vizuri utekelezaji ukatiliwa mkazo. “Kwa umri nilio nao uharibifu wa mazingira ni
mkubwa kuliko elimu inayotolewa. Nikiwa mdogo tulikuwa tunachota maji karibu na
nyumbani kadri siku zinavyoenda maji yanazidi kupungua” alisema Mtove.
Mwenyekiti
wa kikosi kazi namba tatu ambaye pia ni Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja
Ayubu alipongeza juhudi za uhifadhi mazingira unaofanywa na kata ya Ifunda.
Aidha, aliagiza uongozi wa kata ya Ifunda kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na
kamati ya mazingira. “Kila kijiji lazima
kiwe na kamati ya mazingira na kamati hizi ziundwe kwa kujibu wa sheria.
Miongoni mwa majukumu ya kamati hizi ni kuangalia na kusimamia vyanzo vya maji
katika maeneo husika. Katika uundwaji wa kamati hizi, uwiano wa kijinsia lazima
uzingatiwe” alisisitiza Ayubu.
Kikosi
kazi cha kurudisha hali ya ikolojia katika bonde la mto Ruaha kiliundwa na
Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan. Kikiwa katika kata ya Ifunda
kiliongea na wajumbe wa jumuiya ya watumia maji bonde dogo la mto Lyandembela,
kukagua chanzo cha maji cha Mkaa, chanzo cha maji cha Kivalali na chanzo cha
maji cha Ihemi.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni