Na
Dennis Gondwe, IRINGA
Halmashauri ya wilaya ya
Iringa imetakiwa kusimamia sheria ya Mazingira vizuri ili kuondoa uharibifu wa
mazingira katika bonde la mto Ruaha mkuu.
Agizo hilo lilitolewa na
mwenyekiti wa kikosi kazi namba tatu cha kunusuru ikolojia ya mto Ruaha mkuu
ambaye pia ni Katibu Tawala mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu wakati kikosi kazi
hicho kilipokutana na timu ya menejimenti ya Halmashauri ya wilaya ya Iringa
jana.
Ayubu alisema kuwa
Halmashauri ya wilaya ya Iringa inakabiliwa na uharibifu mkubwa wa mazingira. “Ndugu zangu, sheria ya Mazingira lazima
isimamiwe ipasavyo. Katika kusimamia vizuri sheria hii wekeni utaratibu mzuri
wa kusimamia sheria hii kwa kuziimarisha kamati za mazingira kuanzia ngazi za
wilaya, kata na vijiji. Kamati hizi zikiimarishwa utekelezaji wa sheria utakuwa
mzuri na wenye kutoa matokeo mazuri zaidi” alisema Ayubu.
Aidha, alizitaka kamati za
Mazingira kutekeleza majukumu yake na kutoa taarifa za kazi kwa mamlaka
zinazohusika. Alisema kuwa utoaji wa taarifa utaziwezesha mamlaka kuwa na picha
kamili ya hali halisi ilivyo na kuwa na uelewa wa pamoja katika kukabiliana na
changamoto za kimazingira.
Ayubu aliitaka Halmashauri
hiyo kuelekeza miradi yote inayoanzishwa katika Halmashauri hiyo kutoa elimu
kwa wananchi juu ya umuhimu wa utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya
maji. Alisema kuwa ipo miradi ambayo imekuwa ikianzishwa pasipo kuwaelimisha
wananchi juu ya utunzaji wa mazingira na kusababisha uharibifu wa mazingira na
vyanzo vya maji.
Aidha, aliitaka
Halmashauri hiyo kuweka mikakati imara ya kutekeleza uhifadhi wa mazingira. “Halmashauri ya wilaya ya Iringa lazima
muweke mikakati madhubuti inayotekeleza katika kusimamia uendelevu wa agenda ya
uhifadhi wa mazingira” alisema Ayubu.
Mwenyekiti huyo alimtaka
Mwanasheria wa Halmashauri kutoa elimu ya kina ya sheria ya Mazingira na
utekelezaji wake kwa kamati ya usalama ya wilaya ili kuiwezesha inapotekeleza
majukumu yake katika usimamizi na uhifadhi wa mazingira.
Kikosi kazi namba tatu kikikagua chanzo cha maji Kivalali kilichopo kijiji cha Bandabichi wilayani Iringa |
Kwa upande wa afisa ardhi
wa wilaya ya Iringa, Donald Mshani alisema kuwa Halmashauri ya wilaya ya Iringa
inakabiliwa na uharibifu mkubwa wa mazingira kutoka na shughuli mbalimbali
zikiwemo kilimo ndani ya mita 60 kutoka kingo za mito na uingiaji wa mifugo
mingi katika eneo ambalo halina uwezo wa kuihudumia. Alisema kuwa katika
kukabiliana na uharibifu huo, halmashauri ya wilaya ya iringa imepanga
kutekeleza mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji vyote vinavyozunguka
eneo la bonde la mto Ruaha mkuu ili uhifadhi wa mazingira uweze kutekelezwa kwa
mujibu wa sheria na kuwa endelevu.
Awali kaimu mkurugenzi
mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa, Abel Mgimwa alizitaja sababu
zinazosababisha uharibifu wa mazingira katika Halmashauri hiyo kuwa ni ukataji
miti ovyo kwa lengo la kuongeza ukubwa wa mashamba na uchomaji miti kwa ajili
ya mkaa. Sababu nyingine alizitaja kuwa ni wafugaji wengi kuingia maeneo ya
ukanda wa chini katika Tarafa za Pawaga na Idodi na wananchi kuanzisha mashamba
mapya jambo linalosababisha kuondolewa kwa uoto wa asili.
Mgimwa alisema kuwa
changamoto hizo suluhisho lake ni mpango wa matumizi bora ya ardhi. Aliongeza
kuwa pamoja na mpango huo, sheria ndogo za vijiji kuhusu hifadhi ya mazingira
kwa vile vijiji ambavyo havina sheria hizo ili utekelezaji wake uzingatiwe
kikamilifu.
Halmashauri ya wilaya ya
Iringa ina jumla ya vijiji 133 kati ya vijiji hivyo, vijiji 61 ndivyo
vimefanyiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni