Na Dennis Gondwe, IRINGA
Baraza
la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC) limeyatoza faini mashamba ya mifugo ya
Tommy na Ndoto jumla ya shilingi milioni 20 kutokana na kukiuka Sheria ya Mazingira
ya mwaka 2004.
Faini hizo zilitangazwa na
wakili wa serikali mkuu kutoka NEMC, Benard Kongola baada ya kikosi kazi namba
tatu cha kunusuru ikolojia ya mto Ruaha mkuu kukagua hali ya uhifadhi wa
mazingira katika mashamba ya mifugo ya Tommy na Ndoto yaliyopo wilayani Kilolo
Mkoania Iringa jana.
Baada ya kitamka faini
hizo, wakili Kongola alisema kuwa Shamba la mifugo la Tommy limetozwa faini
kutokana na kulima mahindi na migomba ndani ya mita 60 kutoka ukingo wa mto Ruaha
mdogo. Alisema kuwa shamba la mifugo la Ndoto limetozwa faini kutokana na
kufanya biashara bila kuwa na cheti ya tathmini ya hali ya mazingira kutoka
NEMC.
Wakili Kongola alisema
kuwa faini hizo zinatakiwa kuwa zimelipwa ndani ya siku 14 toka tarehe ya faini
hiyo. Aliongeza kuwa baada ya siku 14 NEMC wataenda kukagua utekelezaji wa
agizo hilo.
Kikosi kazi hicho kikiwa
katika ukaguzi wa hali ya uharibifu wa mazingira katika shamba la mifugo la
Tommy kilibaini uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na kupandwa miti isiyo
rafiki kwa mazingira na kusababisha kukauka kwa vyanzo vya maji.
Mwenyekiti wa kikosi kazi
hicho ambaye pia ni Katibu Tawala mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alisema “chanzo hiki cha maji ambacho kinaelekea
kukauka lazima kihifadhiwe ili kirudie hali yake ya awali. Miti hii yote ambayo
si rafiki kwa mazingira lazima ikatwe na kupandwa miti ambayo ni rafiki kwa
maji na niletewe taarifa ya utekelezaji ndani ya wiki moja, alisema Ayubu”.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni