Na Dennis Gondwe, IRINGA
Kikosi
kazi namba tatu cha kunusuru ikolojia ya mto Ruaha mkuu kimeridhishwa na
utekelezaji wa agizo la kuondoa migomba isiyo rafiki kwa vyanzo vya maji katika
shamba la mifugo la Tommy diaries lililopo wilayani Kilolo.
Kauli
hiyo ilitolewa jana na wakili wa serikali mkuu kutoka baraza la Taifa la la
hifadhi ya mazingira (NEMC), Benard Kongola baada ya kikosi kazi hicho kwenda
kufuatilia utekelezaji wa agizo la tarehe 24/4/2017 lililomtaka muwekezaji huyo
kuondoa migomba hiyo shambani kwake wilayani kilolo.
Mwanasheria wa NEMC Benard Kongola (kulia) akikaguautekelezaji wa agizo la ukataji migomba ndani ya kingo za mto Ruaha katika shamba la Tommy Diaries |
Kongola
alisema “migomba ambayo si rafiki kwa
vyanzo vya maji ilikuwa imepandwa ndani ya mita 60 kutoka kingo za mto Ruaha
mdogo jambo ambalo ni ukiukwaji wa sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, sehemu ya
57 ibara ndogo ya 1 inayozuia kulima au kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya
mita 60”.
Alisema kuwa walipotembelea shamba hilo kukagua hali ya uhifadhi
wa mazingira na ikolojia ya bonde la mto Ruaha mkuu waligundua uharibifu huo wa
kimazingira na pamoja na kuwapiga faini ya shilingi milioni 10 kutokana na
kulima mahindi na migomba ndani ya hifadhi ya mto na waliwataka kuondoa mazao
hayo yaliyolimwa ndani ya mita 60.
Wakili
Kongola alizitaka mamlaka za serikali za mitaa kusimamia sheria ya Mazingira ya
mwaka 2004 kwa sababu ipo wazi. Alisema kuwa usimamiaji makini wa sheria hiyo
utasaidia kudhibiti shughuli za kibinadamu zinazofanyika ndani ya mita 60
katika nyanzo vya maji jambo linalohatarisha uendelevu wa vyanzo hivyo wilayani
Kilolo.
Ikumbukwe
kuwa shamba la mifugo la Tommy diaries lilipigwa faini ya shilingi milioni 10
kutokana na kulima mahindi na migomba ndani mita 60 kutoka ukingo wa mto Ruaha.
Vilevile, shamba la mifugo la Ndoto pia lilipigwa faini ya shilingi milioni 10
kutokana na kufanya biashara bila kuwa na cheti cha tathmini ya Mazingira
(EIA).
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni