Na.
Dennis Gondwe, KILOLO
Menejimenti ya halmashauri
ya wilaya ya Kilolo (CMT) imetakiwa kulipa kipaumbele suala ya uhifadhi na
utunzaji wa vyanzo vya maji ili liwe endelevu.
Agizo hilo lilitolewa na
mwenyekiti wa kikosi kazi namba tatu cha kunusuru ikolojia ya bonde mto Ruaha
mkuu ambaye pia ni Katibu Tawala mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu jana wakati kikosi
kazi hicho kilipokutana na timu hiyo katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Kilolo.
Mwenyekiti wa kikosi kazi namba tatu Wamoja Ayubu (kushoto) alifuatilia majadiliano ya wajumbe. Kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kilolo, Venance Kihwanga |
Ayubu alisema “kwenye utoaji wa taarifa za wilaya lazima
uzingatie kipaombele cha utambuzi wa vyanzo vya maji na hifadhi ya mazingira
kama inavyoelekezwa katika ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi”. Alisema
ili kufanikisha jambo hilo halmashauri lazima itenge bajeti na kuweka katika
mipango suala la ufuatiliaji na usimamizi wa vyanzo vya maji na uhifadhi wake.
Mwenyekiti huyo aliutaka
uongozi wa halmashauri hiyo kuendelea kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa
uhifadhi na utunzaji wa vyanzo vya maji. Alisema kuwa uelimishaji huo lazima
uwe shirikishi ukishirikisha viongozi wa chama tawala, wadau na ukijikita kwa
viongozi wa kisiasa na kijamii. “Wataalamu
wenzangu lazima tusimame kwenye taaluma zetu katika kutekeleza majukumu yetu
ili kunusuru uharibifu wa mazingira” alisisitiza Ayubu.
Awali Mkurugenzi mtendaji
wa halmashauri ya wilaya ya Kilolo, Aloyce Kwezi alisema kuwa halmashauri hiyo
ina jumla ya vyanzo vya maji 1,630. Alisema kuwa kati ya vyanzo hivyo vya maji,
vyanzo 938 ndiyo vinavyopewa msisitizo mkubwa.
Alisema kuwa halmashauri yake
inakabiliana na changamoto kubwa mbili na kuzitaja kuwa ni uchomaji moto ovyo
misitu na kilimo katika vyanzo vya maji. Alisema kuwa halmashauri yake imejikita
katika kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya maji
na mazingira kwa ujumla.
Aidha, aliongeza kuwa
halmashauri yake inatambua kuwa mpango wa matumizi bora ya ardhi ni njia ya
kutatua migogoro ya ardhi na uhifadhi wa maziringa. “Hadi sasa vijiji 38 kati ya vijiji 109 vimefanyiwaa mpango wa matumizi
bora ya ardhi” alisema Kwezi.
Kikiwa wilayani Kilolo
kikosi kazi hicho kilikutana na kupokea maoni ya kamati ya usalama ya wilaya,
timu ya menejimenti ya halmashauri, wanasiasa na wakulima na wafugaji wakubwa
wa mashamba ya mifugo wilayani humo.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni