Na.
Mwandishi Maalum, Kilolo
Benki ya NMB imeboresha
huduma zake ili kuwanufaisha watumishi wa serikali na sekta binafsi wilayani
Kilolo.
Kauli hiyo ilitolewa na Meneja
wa benki ya NMB wilaya ya Kilolo, Mary Ngallawa alipowasilisha mada ya umuhimu
wa benki ya NMB kwa watumishi wa umma katika maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa
Umma iliyofanyika katika Ofisi ya mkuu wa wilaya ya Kilolo wiki iliyopita.
Ngallawa alisema kuwa
benki yake imeboresha huduma zake na kuingiza sokoni huduma mpya ili
kuwanufaisha wateja wake. Alisema “kutokana
na wateja wetu kuwa na majukumu mengi, sasa kwa kutumia simu yako ya mkononi
unaweza kuhamisha kiasi cha shilingi milioni tatu kwenda akaunti ya benki
yoyote na shilingi milioni tano kwenda benki ya NMB kwa benki ya NMB”
alisema Ngallawa.
Aliongeza kuwa benki yake ina mikopo kwa ajili ya wastaafu
wanaopata pensheni kila mwezi. “Lengo la
mikopo hii ni kuhakikisha wastaafu wanaendelea kunufaika na huduma za benki
yetu kama walivyokuwa katika utumishi wao awali” alisisitiza Ngallawa.
Nae Afisa Mikopo,
Benjamini Mwakibete alisema kuwa benki ya NMB inatoa mikopo ya nyumba kwa riba
nafuu ya asilimia 19 inayohusisha bima ya nyumba na maisha. Alisema kuwa mikopo
hiyo inajumuisha kununua nyumba, kumalizia ujenzi wa nyumba, au kufanya ukarabati
wa nyumba iliyokwisha jengwa. Alisema mikopo hiyo ni muhimu wa mtumishi kwa
sababu mtumishi ana stahili kuishi katika nyumba nzuri na yenye staha.
Aliongeza kuwa mtumishi anaweza kupata mkopo kwa ajili ya kununua nyumba toka
mashirika yanayojenga nyumba na kuuza kwa wafanyakazi.
Mwakibete alisema kuwa
mikopo ya nyumba inayotolewa inaanzia shilingi milioni 10-700,000,000 na
inalipwa kwa mwaka mmoja hadi miaka 15. Alisema ili kunufaika na mikopo ya
nyumba, lazima mkopaji awe na asilimia 10 ya thamani ya kununua nyumba hiyo na
kiasi kinachobaki benki ndiyo itamkopesha mtumishi kupitia shirika la nyumba.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni