Na. Mwandishi Maalum, Iringa
Watumishi
wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa wametakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia
maadili na weledi wa taaluma zao katika kuhudumia wagonjwa.
Wito
huo ulitolewa na Katibu Tawala msaidizi, Sehemu ya Rasilimali watu katika Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Lucas Kambelenje alipokuwa akiongea na watumishi wa hospitali
ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa katika wiki ya Utumishi wa Umma mkoani Iringa.
Katibu Tawala Msaidizi- Utawala, Lucas Kambelenje akiongea na Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa. Kulia ni Mganga Mfawidi na kushoto ni Katibu wa Afya |
Kambelenje
alisema kuwa watumishi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa wanatakiwa kuwa
mfano mzuri katika utoaji wa huduma za afya na tiba. Alisema kuwa hospitali
hiyo ili iwe mfano mzuri katika utoaji huduma, lazima watumishi wafanye kazi
kwa kuzingatia maadili na weledi wa taaluma zao katika kutoa huduma. Alisema
kuwa wananchi wanaoenda kapata huduma hospitalini hapo wanamatarajio makubwa ya
kupatiwa huduma bora hivyo, huduma bora na kauli njema zinawapunguzia machungu
wanayokuwa nayo hata kabla ya tiba. Alisema kuwa maadili mema kwa mtumishi wa
umma ndiyo msingi wa ufanisi katika kazi wanazofanya.
Akielezea
mafunzo kwa watumishi wa umma, Afisa Tawala Mwandamizi katika Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa, Neema Mwaipopo alisema kuwa mwajili ana utaratibu wa kuwapeleka watumishi
wake katika mafunzo ili kuongeza ujuzi na pia kuimarisha ujuzi walionao kwa
ajili ya kuongeza ufanisi na tija katika utendaji wao wa kazi.
“Ili watumishi waweze kupelekwa katika
mafunzo mbalimbali ni lazima taasisi iwe na mpango wa mafunzo kwa mwaka wa
fedha husika. Mpango wa mafunzo unategemea na mahitaji halisi ya taasisi. Hivyo,
mtumishi hawezi kwenda katika mafunzo kama hayupo katika mpango wa mafunzo”
alisisitiza Mwaipopo.
Mwaipopo
aliongeza kuwa mpango wa mafunzo ni muhimu kwa mwajili kwa sababu unasaidia kufahamu
idadi ya watumishi wanaotakiwa kupelekwa katika mafunzo na gharama za mafunzo husika.
Alizitaja aina za mafunzo kuwa ni mafunzo ya muda mrefu kama shahada ya kwanza
na shahada ya uzamili, mafunzo ya muda wa kati kama stashahada na astashahada,
na mafunzo ya muda mfupi.
Wiki
ya utumishi wa umma ilianza kuathimishwa tangu tarehe 16-23/6/217 ikiongozwa na
kaulimbiu isemayo ‘kuimarisha ushirikishwaji wa jamii katika utoaji huduma: vijana
washirikishwe kuleta mabadiliko barani Afrika’.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni