Na.
Mwandishi Maalum, Kilolo
Jamii imetakiwa kutoa
taarifa za vitendo vya rushwa na viashiria vyake kwa Taasisi ya kuzuia na
kupambana na rushwa nchini (Takukuru) ili kuwa na taifa lisilokuwa na rushwa.
Wito huo ulitolewa na Mkuu
wa Takukuru wilaya ya Kilolo, Fuja Ngalo alipowasilisha mada juu ya umuhimu wa
watumishi wa umma kupinga vitendo vya rushwa mahala pa kazi katika wiki ya
Utumishi wa Umma iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa na kufanyika
katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilolo wiki iliyopita.
Ngalo alisema “tunahitaji ushirikiano wa watumishi na
wananchi kwa ujumla kwa sababu sisi kama Taasisi ya kuzuia na kupambana na
rushwa peke yetu hatuwezi”. Alisema kuwa vitendo vya rushwa vinafanyika
katika jamii, hivyo, jamii ina wajibu wa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na
viashiria vyake ili viweze kufanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria za nchi. “Sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba
11 ya mwaka 2007 kifungu cha 39, kinaelezea wajibu wa mwananchi katika kuzuia
na kupambana na rushwa nchini” alisema Ngalo.
Alisema kuwa katika
kutengeneza mazingira rafiki baina ya taasisi hiyo na jamii, imezindua programu
ijulikanayo kama longa nasi kwa namba 113 ambayo mteja atapiga na kuongea moja
kwa moja na Takukuru na kutoa taarifa za vitendo vya rushwa bila malipo.
Nae, Afisa Uelimishaji wa Takukuru
wilaya ya Kilolo, Ezekiel Mwenda alisme kuwa rushwa ni matumizi mabaya ya
madaraka kwa mtumishi wa umma. Alisema kuwa Takukuru wilaya ya Kilolo
itawashughulikia wote watakaojihusisha na vitendo vya rushwa kwa mujibu wa
sheria za nchi.
Aliongeza kuwa wananchi wanakuwa na hofu kutoa taarifa za
vitendo vya rushwa na kufifisha mapambano dhidi ya rushwa. Alisema kuwa katika
kumlinda mtoa taarifa, Takukuru ina mfumo wa kinga kwa mtoa taarifa siku zote.
Ulinzi wa mtoa taarifa kuhusinana na vitendo vya rushwa au ushahidi mahakamani.
“Kifungu 51 (a) kinatoa kinga kutajwa kwa
jina, makazi, au anuani ya aliyetoa taarifa kuhusiana na vitendo vya rushwa kwa
shahidi” alisema Mwenda. Aliongeza kuwa “Takukuru hatufanyi kazi kwa kumuonea mtu bali tunafanya kazi kwa
uthibitisho ili tusimuonee mtu. Tushirikiane kwenye taarifa na kutoa ushahidi
ili kukomesha rushwa wilayani Kilolo” alisema Mwenda.
Katibu Tawala msaidizi, Sehemu
ya Utawala na Rasilimali watu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Lucas Kambelenje
alisema kuwa mkoa uliona ni muhimu kuishirikisha Takukuru katika maadhimisho ya
wiki ya Utumishi wa Umma ili waweze kutoa elimu kwa watumishi ili wawe mabalozi
wazuri katika mapambano dhidi ya rushwa.
“Ni
matarajio yangu kuwa baada ya mada kutoka Takukuru watumishi wote watakuwa na
uelewa mkubwa juu ya vitendo vya rushwa na viashiria vyake” alisema
Kambelenje.
=30=
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni